MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), ameeleza kwamba sababu zake za kuzuia dhamana kwa anayetuhumiwa kutoa taarifa za uongo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamnyange amelishwa sumu, bado zinaendelea.
Mtuhumiwa huyo ni mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Benedict Ngonyani
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Theophil Mutakyawa, alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Aliyasema hayo baada ya mahakama kutaka kujuia kuhusu hati ya DPP ya kuzuia dhamana kwa mshitakiwa huyo.
Awali, kabla ya hakimu kuhoji juu ya hati hiyo, Wakili Mutakyawa alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na akaomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Akijibu kuhusu hati hiyo, Mutakyawa alidai DPP aliwasilisha hati hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ambacho kinampa mamlaka ya kuzuia dhamana.
“Mkurugenzi wa Mashitaka aliwasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa sababu ya maslahi ya umma na usalama wake. Sababu hizo zinaendelea,” alidai.
Wakili huyo alidai hati ya DPP inaweza kuondolewa mahakamani katika mazingira ya Mkurugenzi wa Mashitaka mwenyewe kuamua kuiondoa au shauri limeisha mahakamani.
Mutakyawa alidai sababu alizozitoa DPP za kuzuia dhamana bado zipo hivyo anaona mshitakiwa huyo aendelee kubaki ndani.
Wakili wa mshitakiwa huyo, Kessi Emmanuel, aliendelea kusisitiza mshitakiwa apewe dhamana.
Alidai mamlaka ya DPP hayawezi kushinda mamlaka ya mahakama katika kutenda haki na pia mshitakiwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili DIT.
Hakimu Mwijage alisema atatoa uamuzi kushokutwa wa kuondoa au kutoondoa zuio hilo la DPP.
Ngonyani anadaiwa kutenda kosa hilo, Septemba 25, mwaka huu, Dar es Salaam.
Anadaiwa kwamba alisambaza taarifa za uongo kupitia mitandao ya WhatsApp na Facebook kuwa Jenerali Mwamunyange amelishwa sumu na kwamba amepelekwa Nairobi Kenya kwa matibabu.