MWANAMUZIKI mkongwe kutoka Afrika Kusini, Dorothi Masuka, amewataka wasanii wanaotoka nchi za Afrika wasisahau kusifia bara lao la Afrika kwa kutaja majina ya nchi wanazotoka tu.
Mkongwe huyo aliliambia MTANZANIA kwamba, wasanii wengi huwa wanatumia muda mwingi kutangaza majina ya nchi zao wanasahau kuitangaza Afrika ili kuimarisha mshikamano wa umoja na utaifa wao.
“Ukiwa Afrika unatakiwa kujivunia na kujitangaza sisi sote ni wasanii kutoka Afrika, kwanini huwa hatujinadi hivyo tunasema mimi natoka Kenya, Tanzania, Nigeria, Ghana, Uganda kwanini tunasahau Afrika wakati wote ni wa Afrika,’’ alieleza mkongwe huyo.
Anasema anapokuwa katika matamasha huwa akifurahia kujitangaza kwamba anatoka Afrika licha ya kwamba anatoka Afrika Kusini kwa baba yake na Zambia kwa mama yake.