Na PENDO FUNDISHA-MBEYA
NAIBU Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson jana aliongoza mamia ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya kushiriki mazishi ya aliyekuwa Diwani wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Esther Mpwiniza.
Mbali na Dk Tulia, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa, (BAWACHA) Halima Mdee alishiriki mazishi hayo na kueleza kuwa chama kilivyopata pigo kutokana na kifo cha Esther, kutokana na mchango wake wa maendeleo kwenye ndani ya chama na kwa jamii nzima ya watanzania.
Katika mazishi hayo, yaliyofanyika jana eneo la makaburi la Saba Saba Jijini hapa, wananchi mbalimbali hususani wafuasi wa chama hicho walijitokeza kwa wingi kushiriki mazishi ya mpiganaji huyo ambapo kifo chake kinatajwa kwamba kimetokana na shinikizo la damu .
Katika salamu zake Mdee alielezea jinsi chama kilivyopata pigo kutokana na msiba huo. Alisema marehemu alikuwa na mchango mkubwa wa maendeleo ndani ya chama na kwa jamii nzima ya watanzania.
Alisema umefika wakati ambao asiwepo raia wa Tanzania ambaye uhai wake utakatishwa kwa kupigwa risasi kama ilivyotokea jaribio la Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu (Chadema) ambaye yupo nchini Kenya kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), alimpongeza Dk. Tulia kwa kitendo chake cha kushiriki mazishi ya kada huyo huku akikitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuweka itikadi za vyama pembeni wakati wa matatizo.
“Msiba hauna itikadi, napenda salamu hizi zifike ndani ya CCM na Serikali kwa ujumla iache kuwazuia wananchi kushirikiana misibani,”alisema Sugu.
Kabla ya kukumbwa na mauti, Diwani Mpwiniza aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema Wilaya ya Mbeya kwa kipindi cha miaka sita.
Pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Fedha katika Baraza la Halmashauri Jiji la Mbeya, Mjumbe wa ALAT Mkoa na Mwenyekiti wa madiwani wanawake Wilaya ya Mbeya.