30.1 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

ATAKAYETOA FEDHA KWA OMBAOMBA KUKIONA

NA MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

MANISPAA ya Ilala imesema tayari imekamilisha mchakato wa kuandaa kanuni ndogo za sheria zitakazotoa adhabu kwa anayetoa fedha kwa ombaomba na mpokeaji.

Akizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki, Ofisa Ustawi wa Jamii, Joyce Augustino, alisema sheria hiyo tayari imekamilika na imekabidhiwa kwa hatua zaidi.

Alisema sheria hiyo inaelekeza mtu anayetaka kutoa msaada auelekeze makao maalumu yaliyotengwa kuwasaidia wasiojiweza.

Joyce alisema manispaa hiyo ina makao manane, ambayo yapo maeneo mbalimbali, yanayohudumia vijana, wazee na watoto wadogo, hivyo kama kuna mtu anahitaji kutoa msaada ataelekezwa aende huko.

“Kuanzishwa kwa sheria hii kutatoa adhabu kwa yeyote atakayepatikana anatoa au kupokea fedha kwa ombaomba, kwani ili kukomesha vitendo hivi ni lazima sheria ichukue mkondo wake,” alisema Joyce.

Alisema wamelazimika kutumia sheria hiyo, kwani wana imani kuwa kuendelea kutoa fedha kwa watu hao kutakuwa kunachangia ongezeko la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Alisema utafiti mdogo walioufanya ndani ya manispaa hiyo, wamebaini watoto wengi wanaoishi katika mazingira magumu wanatoka Bahi, mkoani Dodoma, hivyo ni muhimu viongozi kujenga ushirikiano ili kutokomeza vitendo hivi.

Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Kituo cha Mkono, Manispaa ya Ilala, Suphian Mndolwa, alisema watoto wanaopokewa katika kituo hicho ni wale waliofanyiwa ukatili wa kingono.

Utoaji elimu ya kumlinda mtoto dhidi ya ukatili umepunguza vitendo vya ukatili wa kingono na kubakwa kutoka asilimia 32 Januari hadi kufikia asilimia 19 Machi, mwaka huu.

Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii na Vijana, Fransisca Makoye, amesema ni vyema jamii ikapinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles