Ramadhan Hassan -Dodoma
NAIBU Spika Dk. Tulia Akson ameongoza mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Sumve Richard Ndassa (61), ambaye alizikwa jana Sumve mkoani Mwanza.
Marehemu Ndassa alifariki juzi jijini Dodoma ambapo Spika wa Bunge Job Ndugai juzi alisema ni lazima mbunge huyo azikwe nyumbani kwake Sumve.
Jana mara baada ya kuanza na dua ya kuliombea Bunge na taifa kusomwa ikiwa ni kabla ya bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuwasilishwa bungeni, Spika wa Bunge Ndugai, alisimamana kusema Naibu Spika Dk. Tulia ndiye ambaye ataongoza mazishi ya Ndasa akiwa pamoja na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM).
“Niwataarifu mwili wa Richard Ndassa ndio umewasili pale Sumve muda huu (jana saa nane na robo) kwahiyo jioni hii mazishi yatafanyika waliondoka (Dodoma) saa 6 usiku wa kuamkia leo (jana) tumewakilishwa na Ngeleja na Naibu Spika tunawatakia kila heri katika jambo hilo wanalotuwakilisha,” alisema Ndugai.
Ndassa anakuwa mbunge wa nane kufariki kwa kipindi cha miaka mitano tangu kuanza kwa bunge la 11.
Wengine waliofariki ni Mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Rashid Akbar, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk. Getrude Rwakatare, Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Majimarefu, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Dk. Elly Macha, Mbunge wa Dimani (CCM), Hafidh Ally Tahir, Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama na Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema).
Juzi Ndugai akitangaza kifo hicho, alisema “kwa masikitiko makubwa naomba kuwajulisha bunge letu limepatwa na msiba mwingine mkubwa wa kuondokewa na Mbunge mwenzetu Mbunge wa Sumve Richard Ndassa mbaye amefariki usiku wa kuamkia leo hapa Jijini Dodoma.
“Kufuatia msiba huo tulioupata taratibu mbalimbaliza za mazishi zimeanza kufanyika kwa mawasiliano ya upande wa Serikali na familia. Na kila tukipata taarifa tutafanya hivyo,”alisema.
Atazikwa kijijini kwake
Ndugai alisema ofisi yake itahakikisha mbunge huyo leo jioni (jana) anazikwa katika kijiji chake huko, Sumve.
“Tutajitahidi sana iwezekanavyo kuhakikisha kwamba mheshimiwa huyu, ndugu yetu anazikwa kule Sumve kesho (jana) jioni ‘unless’ tumekuwa advice otherwise (tumeshauriwa vinginevyo) kwa sababu kwa mila zetu za kiafrika kweli kumzika mtu popote linatupa shida.
“Fikiria yeyote ambaye upo hapa unapatwa na jambo kama hilo halafu unawekwa popote, kwahiyo tutajitajidi sana ofisi yangu itashirikiana na Seriklai kuona kila kinachowezekana kinafanyika,”alisema.
Akizungumzia Ndassa, Spika alisema aliingia bungeni mwaka 1995 ambapo na kwamba amelitumikia Bunge kwa kipindi cha miaka 25 kwa vipindi vitano tofauti.