26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Dk. Slaa: Mazingira ya kifo cha Ballali utata mtupu

Aliyekuwa Gavana wa BOT Daudi Balali
Aliyekuwa Gavana wa BOT Daudi Balali

Na Waandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa ambaye anabaki katika kumbukumbu kama kinara wa mapambano dhidi ya fedha za Serikali zilizochotwa Benki Kuu (BoT) na mmoja wa wale waliomtuhumu moja kwa moja aliyekuwa Gavana wa benki hiyo, Daudi Ballali, bado anaamini kuwako kwa mazingira tata kuhusu kifo chake.

Katika mahojiano yake ya hivi karibuni na MTANZANIA, Dk. Slaa alisema bado anaamini kwa asilimia 95 kuwa kifo cha Ballali kina utata mkubwa.

Alisema kama atakuwa hai basi huenda Serikali itakuwa imemficha kwa lengo la kupoteza ushahidi wa wizi wa fedha hizo za EPA.

Wakati, Dk. Slaa akitoa kauli hiyo, MTANZANIA katika kile iliichokiita tangu mwanzo wa ripoti hii Maalumu kuwa wingu jeusi lililojificha kuhusu kifo cha Ballali, katika uchunguzi wake ambao baadhi ya maelezo yake yamethibitishwa na ndugu wa karibu wa Ballali unaonyesha kuwapo kwa hali ya utata ya kifo chake.

Habari kutoka nchini Marekani na kwa ndugu wa karibu wa Gavana huyo wa zamani zinaeleza kuwa kabla ya mauti hayajamkuta Ballali Mei 16, mwaka 2008, alifanyiwa upasuaji na jopo la madaktari waliokuwa wakimtibu ambapo alikatwa sehemu ya utumbo iliyodaiwa kuharibiwa na kitu ambacho hadi sasa kimeacha wingu la mashaka na kisha kuungwa.

Inaelezwa kuwa ndugu wa karibu na Ballali walidokezwa juu ya jambo hilo na inasemekana kwa kiasi kikubwa lilimsononesha Ballali ambaye alidai kusalitiwa na baadhi ya watu.

“Tulielezwa wazi na daktari aliyekuwa akimtibu, lakini nao katika jitihada zao walifanikiwa kumfanyia upasuaji kwa kumkata sehemu ya utumbo na kisha kuunga,” alisema mmoja wa watu aliyeshiriki kumuuguza Ballali.

Katika mahojiano yake na gazeti hili, Dk. Slaa ambaye shinikizo lake ya kuitaka Serikali ichukue hatua kutokana na usiri juu ya suala hilo ndilo lililomsukuma Rais Jakaya Kikwete amfukuze kazi Ballali Januari 9, 2008 miezi mitano kabla ya kifo cha Ballali, wakati huo akiwa tayari ni mgonjwa nchini Marekani.

Dk. Slaa alisema kutokana na utata wa kifo cha Ballali, yeye amekuwa na mawazo mbalimbali kuwa huenda alidhuriwa kwa lengo la kupoteza ushahidi au siku zake zilitimia.

“Mimi huwa nasoma novel na wanaosoma novel watakuwa wananielewa namna movie inavyokuwa… Siku zote fedha haziwezi kutoka hazina bila Gavana kuidhinisha hivyo ukitaka kupoteza ushahidi ni lazima aliyesaini aondoke….Ballali alikuwa wa kwanza kusaini fedha hizo za EPA, hivyo Serikali iliogopa kwenda kumhoji kwa kuwa angewataja vigogo wakubwa serikalini,” alisema Dk. Slaa katika mahojiano yake na gazeti hili.

Dk. Slaa alisema marehemu huyo ndiye mtu pekee aliyekuwa na ushahidi wa kutosha uliokuwa ukihitaji kuwatia mbaroni wale wote waliohusika na wizi wa fedha za EPA, hivyo Serikali kushindwa kumfikia alipokuwa mgonjwa kitandani nchini Marekani na kuchukua ushahidi wake kunajenga mazingira yenye utata wa kashfa nzima.

Hata hivyo, alipoulizwa kama anaamini msingi wa kile alichopata kukisema kuwa Ballali yuko Malta akila raha tofauti na taarifa zilizokuwepo kuwa amefariki dunia, Dk. Slaa alikana kuwahi kuzungumza lugha hiyo.

“Sikupata kusema hivyo. Nilishasema issue si Ballali bali issue ni Serikali ya Tanzania ilipopewa ushahidi lakini ikakataa kufanyia kazi tangu yupo hai na leo wanasema amefariki na walikuwa wanajua kila kitu kwanini walikataa kwenda kumhoji, ni wazi walikuwa wanaogopa kuumbuliwa.

Mimi huwa naamini kwamba, Ballali alipelekwa kufichwa kwa sababu Gavana huwezi kutoka ndani ya nchi yako, haiwezekani Rais asijue na usalama wa taifa usijue vinginevyo nchi hii haina usalama wa taifa na tunaweza tukapinduliwa,” alisema Dk. Slaa.

Katibu Mkuu huyo wa Chadema ambaye anaaminika kuifahamu hoja hiyo ya EPA kutokana na kuvujishwa na kundi dogo la usalama baada ya vigogo wanaodaiwa kuchota fedha hizo BoT kuanza kusalitiana, ndiye aliyekuwa wa kwanza kumshitaki Ballali bungeni katika hotuba yake aliyoisoma kwa niaba ya kambi ya upinzani kuhusu makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2007/2008.

Ni mwendelezo huo wa kelele za Dk. Slaa kwamba, Ballali kwa wadhifa wake wa Gavana wa BoT alizembea au alihusika moja kwa moja na matumizi mabaya ya fedha za Serikali ndani ya taasisi nyeti kwa uchumi wa taifa aliyokuwa akiiongoza ndizo zilizomjengea mazingira Rais Jakaya Kikwete kutangaza kumfukuza kazi Ballali.

Ikiwa ni takribani miaka sita tangu kitokee kifo cha Ballali na tuhuma dhidi yake ziibuliwe bungeni, mtazamo wa Dk. Slaa kwa sasa ni kama ufuatavyo;

MTANZANIA: Ikiwa imepita miaka sita tangu ulipoongoza wabunge wa upinzani kuibua ufisadi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) unaweza kuwaambia Watanzania ni namna gani mlipata vikwazo kutoka serikalini na bungeni kuhusu matakwa yenu ya kutaka uchunguzi kuhusu kashfa hiyo?

DK. SLAA: Nashukuru sana kwa swali lako zuri. Ni kweli nilipeleka hoja hiyo ndani ya Bunge, lakini kwa bahati mbaya sisi wabunge wa upinzani tulipata vikwazo vingi sana kutoka kwa wabunge wa CCM pamoja na mawaziri wao huku wakisaidiwa na Spika wa Bunge wa wakati huo, Samuel Sitta.

Kikwazo cha kwanza walitaka niondoe hoja niliyoitoa pamoja na kwamba nilikuwa na ushahidi wa kutosha.

Ikiwa hilo halitoshi, Sitta alikwenda katika Viwanja vya Mwembeyanga, jijini Dar es Salaam huku akiwatangazia Watanzania kuwa nyaraka nilizozitoa ni ‘feki’ hivyo natakiwa nikamatwe na nifikishwe mahakamani na wakati anazungumza katika mkutano huo ulikuwa ukirushwa moja kwa moja na TBC.

Nilishangaa kwa spika ambaye ni mtetezi wa Watanzania kuongea vitu vya uongo kwa nia ya kuibeba Serikali. Sitta alikuwa anajua kabisa kuwa nilikuwa nikimkabidhi karatasi moja baada ya nyingine tena kabla sijatoa nyaraka zote bungeni sasa baadaye akaja kuumbuka mwenyewe na nashangaa bado hajawaomba radhi Watanzania kwa kusema uongo.

MTANZANIA: Nyaraka hizo wewe ulipewa na nani?

DK. SLAA: Nyaraka hizo nilizipata ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na nilipewa na baadhi ya Watanzania wema ambao wanafanya kazi pale na nia yao ilikuwa kuokoa mabilioni ya wananchi yaliyokwapuliwa na mafisadi na walinipatia nyaraka zote za ufisadi wa EPA.

Kilichonishangaza baada ya mimi kutoa zile nyaraka nilitegemea Serikali ingewatafuta wezi wa zile fedha, lakini badala yake ikawa inawatafuta walionipatia ushahidi.

Nadhani unakumbuka wakati huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Philip Marmo, nilimpelekea nyaraka lakini akasema nyaraka zile za kughushi hivyo kutaka nikamatwe. Nilimwambia Marmo na yeye atakuwa mtuhumiwa namba moja kukamatwa.

Kitu ambacho sisahau mpaka leo na siwezi kufuta kauli hiyo ni kwamba, aliyesaini zile fedha ni Ballali, wakati ule wakasema kuwa Ballali yupo Marekani anaumwa nikasema kwa kuwa aliyeidhinisha fedha kutoka ni yeye hivyo waende wakamhoji kitandani ili tuweze kupata taarifa yake kwa sababu akishafariki hatutakuwa na ushahidi muhimu, wakasema mkono wa Serikali ni mrefu sasa leo wanasema amefariki.

Katika hili sisi tutaendelea kuamini kwamba, Serikali ilishindwa kwenda kumhoji kwa kuogopa kwa kuwa angewataja wakubwa serikalini.

MTANZANIA: Unadhani ni kwanini aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo, Samuel Sitta aliita ushahidi wenu kuwa hauaminiki kwa sababu ni wa mtandaoni?

DK. SLAA: Sitta alikuwa anailinda Serikali. Wakati nakabidhi kitabu changu kwa Sitta document ile ilionyesha akaunti hiyo ilikuwa imesainiwa siku ya sikukuu ambapo benki huwa hazifanyi kazi hapo ndio tuliposhangazwa. Sitta alikuwa anailinda Serikali yake kwa kuwa yeye ni mwanaCCM, huwa anaikimbia Serikali yake pale tu anapoumizwa yeye ndio maana mimi huwa namwita mnafiki siku zote.

Sitta huyu huyu ambaye huwa anasema anapambana na mafisadi alikwenda pale Mwembeyanga na kuwatangazia Watanzania kwamba nyaraka zangu ni feki na baadaye ilipogundulika kuwa ni kweli hadi leo hajawaomba msamaha Watanzania kwa kitendo chake cha kusema uongo.

MTANZANIA: Shutuma mlizozielekeza kwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Daudi Ballali kuwa alihusika na wizi huo mpaka sasa unaamini kuwa zilikuwa na ukweli?

DK. SLAA: Mpaka kesho nitaendelea kuamini kwamba, Ballali alikuwa na share (hisa) zake kwa sababu nyaraka zile zilionyesha kuwa ana akaunti wapi na wapi.

Mpaka leo nashangaa ni kwanini sijakamatwa kama ambavyo kina Sitta na Marmo walipata kusema kuwa ninapaswa kufikishwa mahakamani.

Hivyo kwa kuwa mimi Dk. Slaa, sijakamatwa hadi leo tutaendelea kuamini pasipo shaka yoyote kuwa taarifa nilizozitoa zilikuwa na ukweli asilimia zote.

MTANZANIA: Bado unaamini kuwa sehemu ya fedha zilizokwapuliwa EPA zilitumika katika kampeni za CCM?

DK. SLAA: Ushahidi tulionao sisi katika kipindi hicho cha kampeni Sh bilioni 40 zilichukuliwa ndani ya wiki tatu, huku Sh bilioni 25 ikitolewa kwa siku moja kwenye matawi sita ya Benki ya CRDB na baadaye fedha hizo zikasambazwa sehemu mbalimbali kwa ajili ya kampeni za uchaguzi.

Usikose kufuatilia kesho juu ya kile kilichomkuta Ballali wakati alipokwenda mkoani Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles