24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa wataka Kikwete naye aombewe

Dk. Wilbrod Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa

Na Michael Sarungi

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, amesema Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuombewa na viongozi wa dini kutokana na kuingilia mchakato wa Katiba Mpya.

Kauli ya Dk. Slaa imekuja siku moja baada ya Rais Kikwete kuwaomba viongozi wa dini bila kujali itikadi zao kuwaombea viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili warudi bungeni.

Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alisema kauli ya Rais Kikwete imetolewa kisiasa zaidi na iliyojaa itikadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Kama ni kuombewa basi Rais Kikwete ndiye anayetakiwa kuombewa kwa sababu yeye ndiye aliyeingilia mchakato wa Katiba Mpya siku alipokwenda kuzindua Bunge Maalumu la Katiba.

“Nimeshtushwa mno na kauli hii, umefika wakati wa Rais kutofautisha masuala ya kitaifa na kisiasa zinaelekea kuwa za chama fulani.

“Ombi hili linaonyesha Rais Kikwete anataka kuuhadaa umma wa Watanzania, tunahitaji uimara katika hili, lazima ajue mamilioni ya fedha za Watanzania zinateketezwa,” alisema Dk. Slaa.

Alisema Katiba ndiyo sheria ya msingi katika nchi yoyote ile hivyo kuna kila sababu ya mchakato wake kuheshimiwa.

Alisema Ukawa wako tayari kurudi bungeni iwapo mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba yataheshimiwa.

Kwa upande wake aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel Lwaitama, alisema anamshangaa Rais Kikwete kutokana na kuonyesha upande wa chama chake.

Alisema Rais anapaswa kutambua mamilioni ya fedha za walipa kodi wa nchi hii zinavyotumika kulipa posho za wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

“Huu ni wakati wetu Watanzania kuinua vichwa juu na kuhoji uhalali wa huu mchezo wa kisiasa wa kutaka kuharibu mchakato mzima wa Katiba Mpya,” alisema Lwaitama.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Bashiru Ally, aliwapongeza Watanzania ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba Ukawa warudi bungeni.

Kwa msingi huo, alisema ombi la Rais Kikwete ni muhimu kwa ajili ya mustakabali wa nchi.

“Lazima tuwe na utamaduni wa kutatua matatizo yetu sisi wenyewe, Rais ametoa ombi inabidi lifanyiwe kazi.

“Lazima tuwe na misingi imara ya kujiamulia mambo yetu, hatuwezi kusubiri watu kutoka nje kuja kutufundisha kupatana tunapotofautiana kwa hiyo hizo juhudi za Rais ni nzuri,” alisema.

Alisema ni bora sasa Watanzania wa rika mbalimbali wakaungana ili kuhakikisha wanaendelea kuwa wamoja na wasikubali kuyumbishwa.

Juzi akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya miaka 75 ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) yaliyofanyika jijini Mbeya, Rais Kikwete aliwataka viongozi wa dini bila kujali dini zao kuwaombea Ukawa ili waondokane na mapepo machafu yanayowasababisha kususia vikao vya Bunge la Katiba.

Alisema wajumbe wa vyama vya CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ndio waliochafua upepo.

Alisema mpaka sasa hajapokea taarifa yoyote ya wajumbe wa Ukawa kurejea bungeni Agosti 5, mwaka huu.

Alisema yeye na wenzake walibuni wazo na kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ila anashangaa kuona mapepo yameingilia na kuvuruga.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Ni wazi, kila mtu anajua kwamba Rais Kikwete ndo aliyevuruga mchakato siku ya kuuzindua huko Dodoma. Inashangaza hata wasomi a hali juu wanaendelea kuilinda serikali iliyofanya makosa na uwalazimisha Ukawa warud. Mbona hamumwambii JK amekosea na hivi kumpasa kuomba radhi kwa watanzania na kwenda mbali kurekebisha kasoro zilizopo. Hii inanishangaza sana, kweli watanzania tuna shida. Kwa weli wasomi wetu wameshindwa kusaidia kuongoza nchi yetu, wanatisha sana. Mbona wasomi mnaiogopa CCM au hamjuimini, kwa nini hamtafakari na kuchambua channzo cha Ukawa kususia bunge. yaani mnapenda CCM wakaeneleze lugha yao ya matusina kupoteza pesa ya walipa kodi? Hili sikubaliani nalo kabwe, wasomi mjirekebishe, fungueni macho au mnajikomba mkapate vyeo huko mbeleni?

  2. Tatizo hapa bado kuna watu hata rais angewatukana matusi ya nguoni lakini bado tu watasema “Rais, ulimi umeteleza kwani naye ni binadamu”. Kila kukicha unafiki wa Watanzania unazidi kudhihiri. Tunaelewa kuna watu wanafukuzia vijinafasi ili kuganga njaa hasa wakati huu maisha yanapozidi kuwa magumu na ukweli ni kwamba mchakato ulishavurugwa toka pale wabunge walipofanywa wajumbe.Vyovyote vile katiba ikipatikana itakuwa tena ya CCM na Wananchi wataendelea kudai yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles