29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo bandari watinga kortini

mgawe
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe, akiwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kufikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka. Picha na Humphrey Shao.

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma, Hamadi Koshuma, wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia madaraka vibaya.

Washtakiwa hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Beny Linkoliny mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Isaya Arufani.

Beny alidai washtakiwa wakiwa katika nyadhifa zao wakiwa TPA, Desemba 5, 2011 walitumia madaraka vibaya.

“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa kwa pamoja kwa kutumia madaraka vibaya walisaini mkataba wa kibiashara kati ya TPA na Kampuni ya Ujenzi ya China kwa ajili ya kujenga geti namba 13 na 14.

“Washtakiwa mnadaiwa mlisaini mkataba huo na kampuni ya China bila kutangaza zabuni ya ujenzi wa geti namba 13 na 14 kwa nia ya kupata faida kutoka kwa kampuni hiyo ya China,” alidai Beny.

Washtakiwa walikana kutenda makosa hayo, upelelezi haujakamilika na upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi kwa washtakiwa kudhaminiwa.

Hakimu Isaya alisema shtaka dhidi ya washtakiwa linadhaminika hivyo watadhaminiwa kwa masharti ya kusaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 2, wadhamini wawili ambao pia watasaini dhamana ya kiasi hicho cha fedha kwa maandishi.

Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana, wako nje kwa dhamana hadi Agosti 13 mwaka huu kesi yao itakapotajwa.

Wakurugenzi hao waliondolewa kazini Januari mwaka jana na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na kuisababishia Serikali hasara kubwa.

Wengine waliotimuliwa kipindi hicho ni aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Miundombinu, Julius Mfuko, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ngamilo, Meneja Kituo cha Kupakulia Mafuta, Tumaini Massaro.

Dk. Mwakyembe alidai Mgawe alizembea na kuruhusu kuwapo kwa muda mrefu utaratibu usiofaa wa upokeaji na uondoshwaji bandarini wa mafuta machafu.

Katika tuhuma hiyo, Mgawe anadaiwa kuachia kiasi kikubwa cha mafuta safi kuibwa na kushindwa kudhibiti kiwango cha utoaji bandarini wa mafuta machafu kinyume na mikataba iliyopo.

Tuhuma ya pili iliyomwondoa Mgawe, ni ufanisi duni ambao Dk Mwakyembe alifafanua kuwa alishindwa kudhibiti wizi uliokithiri bandarini wa mizigo na mali ya Mamlaka.

Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, pia alikiuka sheria na utaratibu ambapo anadaiwa kuingia mkataba na Kampuni ya China Communications Construction Ltd (CCCC) bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni ya Mamlaka.

Pia anadaiwa kuongeza mishahara kwa asilimia 15 Julai mosi mwaka juzi bila idhini ya Waziri wa Uchukuzi, hivyo kukiuka utaratibu uliowekwa na sheria.

Tuhuma zilizomng’oa Koshuma kwa mujibu wa Dk Mwakyembe ni nne; ya matumizi mabaya ya madaraka. Anadaiwa kuruhusu michakato ya zabuni bila kufuata utaratibu kwa kisingizio cha miradi mikubwa.

Koshuma pia anadaiwa kuwa na ufanisi duni, ambapo akiwa Mjumbe wa Bodi ya Zabuni, alishindwa kuijulisha Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi ya Umma (PPRA), kuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi.

Ukiukwaji huo ulifafanuliwa kuwa ni wa kuruhusu Mamlaka kuingia mkataba wa kibiashara na CCCC bila kushirikisha Bodi ya Zabuni na kushindwa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka katika udhibiti na uendeshaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles