29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

UN yamchokonoa Rais Kagame

Paul Kagame
Rais wa Rwanda, Paul Kagame

Patricia Kimelemeta na Oliver Oswald, Dar es Salaam

UMOJA wa Mataifa (UN), umemtaka Rais wa Rwanda, Paul Kagame kuwajumuisha wanajeshi waasi wa kundi la FDRL kwenye jeshi la nchi yake.

Uamuzi huo umetolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.

Membe alisema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha siku tatu kilichowashirikisha viongozi wa umoja huo, Umoja wa Afrika (AU) na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Alisema kikao hicho kilianza Julai 2, mwaka huu na kumalizika Julai 5, mwaka huu nchini Rwanda, kwa pamoja washiriki waliona ipo haja kwa Serikali ya Rais Kagame kuwapokea waasi hao ili kurejesha amani ya kudumu nchini humo.

Alisema kikao hicho kilifanyika kutokana na maombi ya waasi hao ya kutaka kukutanishwa kwenye meza ya mazungumzo na Serikali ya Rwanda ili kumaliza tofauti zao.

Membe alisema pamoja na UN kuushirikisha Umoja wa Afrika na SADC kwenye kujadili barua ya waasi, pia ilizishirikisha nchi zilizopeleka majeshi kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Kikao kilihusisha taasisi mbalimbali za kimataifa na Tanzania tumeshirikishwa kutokana na kuwa moja ya nchi washirika zilizopeleka majeshi ya kulinda amani DRC,” alisema Membe.

Alisema kikao hicho kiliridhia ombi hilo la waasi hata hivyo, kimetoa masharti magumu kwao, ambapo wamewataka kutoka mafichoni kushusha silaha chini na kuwa raia wa kawaida ili waweze kurejeshwa makwao na wengine kujumuishwa kwenye majeshi ya Rwanda.

Alisema endapo waasi hao watashindwa kutekeleza maazimio hayo, majeshi ya UN yatahakikisha yanaanzisha mapigano yatakayowasambaratisha ndani ya muda mfupi.

Alisema wameitaka Serikali ya Rwanda, kuwajumuisha waasi wote watiifu na wenye uzoefu wa kivita kwenye majeshi yake.

Mbali ya mapendekezo hayo, lakini pia Serikali ya Rwanda imetakiwa kuwajengea kambi maalumu waasi wote watakaokosa nafasi kwenye jeshi la nchi hiyo.

Alisema kambi hizo zitakazokuwa chini ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), SADC na Rwanda yenyewe zitatumika kufanikisha mpango wa kuwarejesha makwao na kuwapa nafasi ya kupatiwa msaada wa kibinadamu.

Aliongeza kuwa UN imetaka mapendekezo hayo yatekelezwe ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi huu na kwamba harakati za kumshawishi Rais Kagame kukubali uamuzi huo zinaendelea.

Mapendekezo ya UN yametafsiriwa kuwa ni mtego kwa Serikali ya Kagame, ambaye amekuwa hataki kupokea ushauri wa kufanya mazungumzo na waasi, ingawa kumekuwa na mashinikizo mbalimbali ya kumtaka kumaliza uhasama na waasi hao.

Mwanzoni mwa mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete akiwa kwenye mkutano wa AU wa kujadili amani na mpango wa ulinzi nchini DRC uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia aliitaka Serikali ya Rais Kagame kukaa meza moja na waasi ili kumaliza tofauti.

Ushauri huo wa Rais Kikwete ulimkera Kagame na baadhi ya maofisa wa Serikali yake, ambapo walianza kutoa maneno ya kejeli kwa Serikali ya Tanzania.

Rais Kagame akiwa kwenye sherehe za kuhitimisha mafunzo ya maofisa wa jeshi la nchi yake wapatao 45, alimkejeli Rais Kikwete kwa kusema kuwa ushauri wake ni wa kijinga kwa Wanyarwanda na kwamba ni sawa na kuwachezea.

“Nimekaa kimya kwa kipindi kirefu na kwa jinsi nilivyoweza kwa sababu nilifikiri kwamba mazungumzo ya kipuuzi yaliyozungumzwa na watu wajinga yamemalizika,” alisema Rais Kagame.

Kundi la waasi wa FDRL ni la pili kwa ukubwa katika eneo la mashariki mwa Kongo kuwa tayari kusitisha mapigano.

Kundi la kwanza kufanya hivyo ni lile la M23, ambalo lilisitisha mapambano baada ya kukung’utwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa.

MAUAJI YA PALESTINA YALAANIWA

Kwa upande mwingine, Serikali imelaani vikali mauaji yanayoendelea kutokea katika nchi za Palestina na Israeli.

Alisema Tanzania ikiwa kama mshirika wa nchi hizo, inapaswa kukemea na kulaani vitendo hivyo ili kuzuia umwagaji wa damu unaosababishwa na vita hivyo.

Aliiomba UN kuingilia kati suala hilo na kuzishawishi nchi hizo kuacha vita ili kuepusha athari zinazoendelea ambazo zinasababisha mauaji ya wananchi wasio na hatia.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. wazo la UN nizuri linaonesha ukamavu hususani katika kulaanichokochoko zilizosababisha vita kati ya Israel na Gaza na kusababisha mamia ya raia kupoteza maisha bila kuegemea upande wowote . chokochoko na kukosekana kwa suluhusu kuna madhara na haya ni matokeo yake. sasa mauaji yamewalenga Wazee, watoto, walemavu, wagonjwa na wanawake. kilichosemwa na kuacha watu wengi kukosa makazi. hivi pasingetumika njia mbadala badala ya vita? UN anzisheni secreate ya kuzuia majanga badala ya kusubiri majanga yatokee

  2. siyo mara ya kwanza wana jeshi wa FDLR kuingia kw ajeshi la RWANDA!!!! wengi wameingia wakiisha jisalimika wameingizwa kwa ujumla kwa majeshi ya RWANDA mifani ni nyingi hata majina tunao kama GENERAL RWARAKABIJE na w’askali wengi ameinigia nao hii si shida kwa RWANDA, wale wamemwanga damu nao watfwatiliwa mahakamani hati Kagame akiondoka!!!Tanzania haiwezi chochote kwa ondoa zambi awa wa nterahamwe wametenda RWANDA, isiyo tu kusaidia

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles