27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein: Uchaguzi umekwisha, tuchape kazi

Pg 4Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

HATIMAYE Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameapishwa kushika wadhifa huo na kusema kwamba uchaguzi umekwisha na sasa watu wafanye kazi.

Sherehe hizo zilifanyika jana mjini Unguja katika Uwanja wa Amaan, ambapo viongozi mbalimbali wa kitaifa walihudhuria huku mabalozi wengi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wakishindwa kuhudhuria.

Viongozo waliohudhuria sherehe hizo ni Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akizungumza baada ya kuapishwa, Dk. Shein aliwapongeza washindani wake kwa kukubali matokeo na ameahidi kushirikiana nao katika kuijenga Zanzibar yenye mafanikio.

Aliwataka wananchi kudumisha amani na kuahidi kuwa atatumia uwezo wake wote ili Zanzibar iendelee kuwa na amani na utulivu.

“Serikali zote mbili hazitamvumilia mtu yeyote au kikundi cha watu watakaojaribu kuichezea amani na utulivu uliopo.

“Na ninasema tena hapa uchaguzi umekwisha sasa tufanye kazi ya kuleta maendeleo ya kweli hapa Zanzibar, tunajua haikuwa kazi rahisi kwa ZEC kusimamia uchaguzi lakini Mungu ametujalia tumemaliza salama.

“Ninawahakikisha nitaunda Serikali makini ambayo itafanya kazi kwelikweli kama ilivyo kauli mbinu ya Rais Dk. John Magufuli ya Hapa Kazi Tu!,” alisema Dk. Shein

Tamko la mabalozi Machi 21, mwaka huu, mabalozi na wawakilishi wa nchi za Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Switzerland, Uingereza na Marekani walitoa tamko kuhusu uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar Machi 20, mwaka huu Visiwani Zanzibar.

“Tumesikitishwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wa kuendesha marudio ya uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, bila kuwepo makubaliano ya pamoja baina ya pande kinzani na ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa visiwani humo uliotokana na majadilino baina ya pande husika.

“Ili uwe wa kuaminika na kukubalika ni lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu.

“Tunarejea wito wetu kwa Serikali ya Tanzania kuonyesha na kuchukua uongozi katika suala la Zanzibar na kujielekeza katika kupatikana kwa ufumbuzi wa mgogoro huu kwa kupitia mazungumzo baina ya pande husika kwa lengo la kudumisha amani na umoja katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa mara nyingine tunawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa utulivu na ustahimilivu waliouonyesha katika kipindi chote cha mchakato huu na kuvitaka vyama vyote na wafuasi wao kuanzisha tena mchakato wa maridhiano ya kitaifa ili kupata ufumbuzi jumuishi, endelevu na wa amani,” ilieleza taarifa hiyo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles