Na Muhammed Khamis (UoI)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amevunja ukimya na kusema kuwa hakuna Rais mwingine wa Visiwa hivyo ila ni yeye ambaye anatambuliwa kwa mujibu wa Katiba.
Amesema hatamzuia aliyekuwa mgombeas urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuzungumza, akisema licha ya kueneza propaganda za kufanyika mabadiliko ya uongozi hakuna lolote litakalofanyika hadi mwaka 2020.
Kauli hiyo aliitoa mjini Unguja jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani Machi mwaka jana.
Dk. Shein alisema licha ya baadhi ya wanasiasa kueneza kila aina ya maneno mitaani visiwani humo kuhusu mabadiliko katika uongozi hakuna mabadiliko yoyote yatakayofanyika.
Alisema ni kawaida na hata Katiba ya nchi inatambua uhuru wa mtu kuzungumza kile anachokipenda ili mradi tu asivunje sheria za nchi.
Hata hivyo, alisema wapo wanasiasa wamekuwa wakitumia kifungu hicho kuzusha maneno ya propaganda mitaani.
“Sitaweza kumzuia Maalim Seif (Katibu Mkuu wa CUF), wala mwingine asiseme jambo lake maana anayo haki ya kufanya hivyo.
“Lakini nataka niwahakikishie tu kuwa Zanzibar hakutakuwa na mabadiliko ya uongozi wala uchaguzi mwingine hadi mwaka 2020,” alisema Dk. Shein.
Alisema hakuna asiyejua kuwa yeye ndiye rais wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba na mamlaka inayoweza kumthibitisha ni Tume ya Uchaguzi pekee na si mtu mwingine yoyote.
Akizungumzia mwaka mmoja wa uongozi wake, Rais Dk. Shein, alisema Serikali imepiga hatua kubwa ya maendeleo tangu ulipomalizika Uchaguzi Mkuu Machi mwaka jana.
“Kuwapo amani na utulivu visiwani hapa ni miongoni mwa sababu kubwa zinazoifanya Serikali kukusanya kodi kwa kiwango kikubwa zaidi ikilinganishwa na miaka ya iliyopita,” alisema.
Aliwataka wananchi wa Zanzibar kujikita zaidi katika kufanya kazi kwa sababu ndiyo silaha ya kujikwamua katika uchumi badala ya kupiga maneno yasiyokuwa na tija.
Akieleza kuhusu mikakati mipya ambayo Serikali imedhamiria kuitimiza, alisema ni pamoja na kuhakikisha ina wataalamu wa kutosha ambao watakuwa wazalendo wa visiwa hivyo kuepusha changamoto za aina tofauti ambazo zimeonekana kujitokeza kwenye baadhi ya wizara kwa watendaji wake.
Dk. Shein alisema anasikitishwa na vitendo vilivyokithiri vya udhalilishaji wanawake na ubakaji wa watoto, vitendo ambavyo Serikali haiwezi kuvifumbia macho.
‘’Katika kuhakikisha tunapambana na hali hii kwa sasa tumezuia dhamana kwa wale wote ambao watakutwa na tuhuma za ubakaji mpaka kesi zao zitakapoamuliwa na Mahakama,” alisema.