Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
Watumishi wa Kitengo cha Figo cha Hospitali ya Taifa Muhimbili, dawati linalohusika kutoa namba kwa wagonjwa wametakiwa kutoa namba kwa wagonjwa bila upendeleo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile ametoa agizo hilo leo Jumanne Machi 13, alipofanya ziara ya kushtukiza katika Kitengo hicho.
Nilikuja kukagua iwapo wametekeleza maagizo ambayo tuliwapatia awali, kumekuwa na maboresho ingawa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa kutoka hadi nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Hospitali ina mashine 42 za kuchuja damu na watumishi wanalazimika kufanya kazi zaidi ya muda wa kazi ambapo kwa siku huona wagonjwa zaidi ya 80 na huduma zinakwenda vizuri.
“Nimewaagiza watumishi dawati la kutoa namba kuzingatia orodha ya utaratibu wa kutoa namba, yule anayefika mapema atibiwe aondoke kwa wakati ili kusiwepo malalamiko na waweke visanduku vya kukusanya maoni, ushauri na malalamiko.
“Pia nimewaagiza waweke luninga ili ziendelee kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa haya na jinsi ya kuyaepuka maana hapa nimeulizwa maswali ambayo kama kungekuwa na luninga nisingeulizwa kwani elimu hiyo wangeipata hapo,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru amesema hospitali hiyo inazidi kuimarisha kitengo hicho na kwamba kwa mujibu wa wataalamu asilimia 60 ya wagonjwa wanaofanyiwa huduma ya kusafisha damu (dialysis) huhitaji huduma ya kupandikizwa figo.