28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mwinyi:Tumeamua kufanya mageuzi ya uchumi

Mwandishi Wetu- Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar,imeamua kufanya mapinduzi ya kiuchumi kwa kuendeleza uchumi wa buluu na kuweka mkazo katika kuziimarisha sekta za huduma, ikiwemo sekta ya utalii, ambayo ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo wakati wa  hafla iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa viongozi waandamizi na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi juzi.

Alisema kutokana na udogo wa ardhi kila uchao zinaendelea kuibuka changamoto katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ambapo ardhi yote ya Unguja ni kilomita za mraba 1,666 na Pemba ni kilomita za mraba 988 ambapo ukubwa huo hauendani na ongezeko la watu.

Alisema zamani ardhi ilitegemewa kwa kilimo na wananchi wengi waliweza kuendesha maisha yao kwa kutegemea shughuli za kilimo na ufugaji ambapo leo ardhi hiyo hiyo inategemewa sana kwa ujenzi wa makaazi, viwanda na shughuli nyengine za uchumi wa karne hii ya 21.

Alisema Serikali imeamua kutumia rasilimali mbadala ya bahari pamoja na kuimarisha sekta za huduma.

Alisema  imelenga kuendesha na kukuza uchumi wa buluu kwa kuzitumia kikamilifu rasimali zinazohusiana na bahari, ikiwemo shughuli zinazohusu sekta ya utalii, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, uvuvi na bahari kuu, ufugaji na usindikaji wa samaki, ukulima wa mwani, pamoja na mazao mengine anuwai ya bahari.

Alimuahidi  Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela kumpa timu maalumu  ya kushirikiana na benki hiyo katika kufanya kazi huku akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imeamua kutoa ushirikiano mzuri kwa  sekta binafsi ambapo imekusudia kwa dhati kuwa wadau wezeshi wa sekta binafsi kwa kuwawekea mifumo rafiki na mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi bila ya kikwazo.

“Nimefurahishwa sana kusikia benki imehamasika kutokana na mwelekeo wa maendeleo na dira yangu ya kuijenga Zanzibar mpya na kuamua kutuunga mkono katika jitihada zetu za kufanikisha malengo yetu tuliyoyakusudia, ahsanteni kwa moyo wenu huo wa kizalendo”,alisema.

Alisema  hamu ya benki  kushirikiana na Serikali hasa katika masuala ya uchumi wa Buluu imemtia moyo na ana imani kubwa kwamba mashirikiano hayo yataongeza kasi ya uzalishaji na sekta zinazotegemea mazao ya baharini kama vile viwanda na usindikizaji vitaibuka na kuimarika.

Alisema dhamira ya Serikali  ni kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo la kimkakati la uwekezaji ambapo pia, Serikali imejipanga kuendeleza utalii, kukuza biashara na viwanda na kushajiisha uwekezaji katika maeneo mapya ya uchumi.

Aliitaka kuwa na ujasiri wa kuwapatia mikopo wananchi wanaojishughulisha katika sekta ya kilimo, uvuvi wa kawaida, ujasiriamali na ufugaji, wauzaji wa biashara ndogo ndogo na za kati  wanahitaji kuwezeshwa zaidi ili biashara zao ziwaletee kipato chenye tija itakayoweza kuwakwamua na umasikini.

Aliwataka wafanyabiashara na wananchi wote wenye fedha nje ya nchi kuzileta fedha hizo nyumbani ili waweze kuijenga nchi yao na kuwaahidi kwamba hawatahojiwa wala kubughudhiwa kwa aina yoyote. “Tunataka kuijenga nchi yetu na nchi hujengwa na wananchi wenyewe.

Nsekela akiwasilisha mada juu ya shughuli za benki hiyo na jinsi ilivyojipanga katika kushirikiana na Serikali na kueleza iko tayari na kumuomba Rais aipe timu kwa ajili ya kufanya kaziili kuleta maendeleo ya kasi na chanya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles