25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi, wananchi kukomesha mauaji ya vikongwe

Abdallah amiri, Igunga

JESHI la Polisi wilayani Igunga mkoani Tabora kwa kushirikiana na taasisi za dini na wananchi, wamejipanga kukomesha vitendo vya kikatili yakiwemo mauaji ya vikongwe vinavyoendelea kuongezeka katika wilaya ya Igunga.

Kauli hiyo, ilitolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga (OCD), Ally Mkalipa wakati akizungumza na wananchi na wanafunzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja cha kumbukumbu ya Sokoine mjini Igunga, wakati wa ye uzinduzi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Alisema pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali za kutoa elimu kwa wananchi kuacha tabia ya kujihusisha na vitendi vya ukatili lakini bado vimekuwa vikiendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Alisema kutokana na hali hiyo, jeshi  hilo limejipanga kukomesha vitendo hivyo kwa kutoa elimu katika shule zote na kufanya mikutano katika ngazi ya vitongoji, vijiji, kata na tarafa ikiwa pamoja na kuzishirikisha taasisi zote za dini pamoja na kuwasaka na kuwafikisha mahakamani kwa wale wote watakaobainika kuendelea na vitendo hivyo vya ukatili.

“Wananchi na wanafunzi mliokusanyika hapa,tunawaomba mtupe ushirikiano kwa kutoa taarifa polisi pindi mnapowabaini watu wanaojihusisha na vitendo vya ukatili kwani sisi peke yetu hatuwezi kufanikisha vita,” alisema.

Alitoa wito kwa wanafunzi wote wilaya nzima kuepukana na zawadi au kupewa lifti na watu wasiowatambua, kwani wapo baadhi yao sio watu wema.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Igunga, Brainer John alisema kuanzia  Januari  hadi Septemba, mwaka huu, kesi zimeripotiwa 133, kati ya hizo zilizopelekwa mahakamani ni 52 zilizo chini ya upelelezi ni 81,zilizopatiwa hukumu ni 20 sawa na ongezekeo la makosa 15, ikilinganishwa na  mwaka jana ambapo yaliripotiwa makosa yalikuwa 118.

Alisema wilaya hiyo, ina vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani kwa wanawake, wazee na wasichana kama mauaji ya vikongwe, vipigo na mashambulizi, ndoa za utotoni, ubakaji, ulawiti, lugha za matusi, ushiriki hafifu katika maamuzi ya familia na kusema kuwa jeshi la polisi limekuwa likichukua hatua kwa wale wote wanaojihusisha na maswala ya vitendo vya ukatili.

Kaimu Mganga Mkuu  Wilaya ya Igunga, Sala Kilakuno alisema kutokana na watoto wadogo kupata mimba za utotoni, wamekuwa wakipata shida wanapojifungua kwa sababu viungo vyao vinakuwa havijakomaa.

Hakimu Mkazi Wilaya ya Igunga, Jackline Kessy aliwataka wananchi kwenda kutoa ushahidi mahakamani pindi washtakiwa wanapofikishwa mahakamani ili haki itendeka kwa kuwa bila ushahidi watuhumiwa wanaweza kuachiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles