24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mwigulu atoa siku 90 halmashauri kulipa wazabuni

Na Waandishi Wetu, Dodoma

HALMASHAURI zote nchini zimeagizwa kuhakikisha zinalipa madeni ya wazabuni na  watoa huduma ndani ya miezi mitatu kabla ya kumalizika kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022 Septemba mwaka huu.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu marekebisho ya tozo  ya miamala ya simu baada ya kusaini marekebisho ya kanuni hizo jana.

“Rais anaguswa sana na madeni ya watoa huduma hasa watoa huduma wadogo, fedha zao kukaa Serikalini kwa muda mrefu, wengine walikopa kwenye mabenki na wengine wameshapata misukosuko, Rais ameagiza walipwe haraka”, amesema Dk. Nchemba.

Amesema watoa huduma hao walipwe haraka ili fedha hizo ziingie kwenye mzunguko kwa kuwa kutokuwalipa ni sawa na kuwatia umasikini kitu ambacho si lengo la Serikali.

Kuhusu tozo za miamala ya simu amesema hadi Agosti 31, 2021 Serikali imekusanya jumla ya sh. bilioni 63 ambazo zitatumika kwa ujenzi wa vituo vya afya 220 katika Tarafa zote 220 ambazo hazijawahi kuwa na huduma hiyo tangu nchi ipate uhuru.

Amesema fedha zitakazokusanywa kutoka katika tozo hizo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa zitatumika kwa ujenzi wa madarasa na kununua madawati ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

“Januari mwakani tutaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kuongezeka mara mbili ya mwaka uliopita, si vema tukarudi kule tulikotoka kwa wanafunzi kufaulu 50 halafu anachaguliwa mmoja kutokana na ukosefu wa madarasa”, amefafanua Dk. Nchemba.

Amesema kwa ruhusa aliyopewa na Waziri wa Nchi TAMISEMI, Ummy Mwalimu, amewaagiza madiwani kutoa taarifa rasmi ya mahitaji ya madarasa kwa kila Kata kwa ajili ya wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

Amesema taarifa hizo zitaiwezesha Serikali kugawa fedha kutokana na mahitaji ili kuhakikisha azma ya Rais inayotaka wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa darasa la saba watakaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanadahiliwa.

Imeandaliwa na Regina Frank, Sandra Charles, Rahma Taratibu, (SJMC)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles