Na Mwandishi Wetu -DODOMA
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa viashiria vya uchumi na utekelezaji wa bajeti kwa ujumla na kama itabainika kutakuwa na haja ya kufanya marekebisho itafanya hivyo wakati wa mapitio ya nusu mwaka Desemba.
Akihitimisha kujibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2020-2021, Dk. Mapango alisema Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa viashiria vya uchumi na utekelezaji wa bajeti kwa ujumla.
“Na kama itabainika kutakuwa na haja ya kufanya marekebisho ya bajeti, itafanya hivyo wakati wa mapitio ya nusu mwaka Desemba,” alisema Dk. Mapango.
Alisema Serikali imefuta tozo zaidi ya 60 ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na fedha za kuweza kujikimu wao na familia zao.
“Na mnaona kabisa kwamba tumefanya uamuzi mkubwa wa makusudi, kwamba mwaka ujao wa fedha Julai mosi hatuongezi kabisa ushuru wa bidhaa, tumeshusha kiwango cha ‘skill development levy’, tumefuta tozo takribani 60 na yote tunafanya katika kuhakikisha mfukoni wananchi wetu wanakuwa na fedha zaidi za kujikimu wao na familia zao katika kipindi hiki kigumu,” alisema Dk. Mapango.
Alisema kupitia kaguzi mbalimbali, wamegundua kwamba mamlaka za hifadhi za taifa kuna upungufu mkubwa ambapo Serikali itatatua kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi.
Dk. Mapango alisema Hazina, Wizara ya Maliasili na Utalii na mamlaka za hifadhi zitakaa pamoja kuandaa taratibu za kuhakikisha shughuli nyeti za uhifadhi ikiwa ni pamoja za operesheni za dharura kukabiliana na ujangili.
“Tutafanya hivyo kama ambavyo tunafanya pia kwa ajili ya vyombo vya ulinzi na usalama vingine vyote ambavyo posho zao zinalindwa, na utaratibu huu sio mpya ndio unaotumika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), pia unatumika mamlaka za viwanja vya ndege na inatumika kwa ufanisi,” alisema Dk. Mapango.
Kuhusu ugonjwa wa corona, alisema hakuna athari zozote kwenye uchumi zilizojitokeza na kwamba chakula kipo cha kutosha.
“Kwenye hotuba ya bajeti nilieleza walifanya tathmini ya kiuchumi kati ya Januari na Aprili mwaka huu, ilionyesha kwamba nchi yetu haijaathiriwa sana na ugonjwa wa corona ikilinganishwa na mataifa mengine.
“Mauzo ya dhahabu yaliongezeka kutoka takribani Sh bilioni 743.8 hadi trilioni 1.5 ukilinganisha na mwaka 2019/2020,” alisema Dk. Mapango.