23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Miradi ya Tanesco Geita na Chato kukamilika Oktoba 2020

Mwandishi Wetu

MIRADI ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato inayotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kama Mkandarasi na Mshauri Elekezi inatarajia kukamilika Oktoba 2020.
Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya ofisi za TANESCO katika mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka alisema amefurahishwa na ubora na kasi ya ujenzi huo.

Dk Mwinuka aliyeambatana na viongozi wengine wa menejimenti, wametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya ofisi hizo na kwamba alisema ujenzi wa majengo hayo ni sehemu ya jitihada za shirika, kuhakikisha linaendesha shughuli zake katika majengo yake na hivyo kuepukana na gharama kubwa za upangishaji majengo kwa matumizi ya ofisi za shirika kuanzia ngazi za kanda, mkoa mpaka wilayani.

Alisema lengo hilo linakwenda sambamba na maagizo ya serikali ya kuhakikisha ofisi zote za Serikali, zinajenga na kumiliki majengo ya ofisi zake katika maeneo yote ambako zinaendesha shughuli zake.

“Leo hii nimetembelea kukagua na kujionea ujenzi unaoendelea wa majengo ya ofisi za Tanesco Mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato, ambako yote ujenzi wake unakwenda vizuri chini ya mkandarasi TBA akiwa chini ya usimamizi wa karibu wa Tanesco.

“Nawashukuru TBA na Menejimenti yake kwa kuwa nimekuja kujionea utofauti wa tunayoyasikia na tunayoyaona huku na kwamba nawaagize kuongeza kasi ya ujenzi ili kuwezesha kukamilisha kwa majengo haya mapema zaidi ili shirika liweze kuondokana na matumizi ya nyumba za kupanga kama ofisi na kuhamia katika majengo yake,” alisema Dk Mwinuka.

Naye Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mbunifu Majengo Godfrey Mwakabole, alisema kuwa ujenzi unakwenda vizuri kwa kasi inayoridhisha na kwamba wanatarajia yote mawili kuyakamilisha Oktoba mwaka huu.

“Ujenzi unakwenda vyema na tunapata ushirikiano mzuri sana kutoka Tanesco, na niwaahidi kukabidhi majengo bora na kwa wakati iwezekanavyo na kwamba changamoto zilizopo ni ndogo ndogo ambazo huwa tunakaa vikao vya mara kwa mara na mteja wetu Tanesco na kuzipatia ufumbuzi haraka bila kukwamisha utekelezaji wa miradi hii,” alisema Mwakabole.

Aidha, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Geita, Joachim Ruweta aliisema kuwa kukamilika mapema kwa majengo hayo itakuwa ni moja ya hatua kubwa katika uboreshaji wa huduma za umeme na mazingira ya kufanyia kazi kwa wafanyakazi wao.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles