30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango: Bila uwekezaji endelevu hakuna kodi

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amewaomba washiriki wote wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji mwaka 2024 kutoa maoni na mapendekezo kwa uhuru ili waweze kuboresha zaidi sera za kodi na uwekezaji nchini huku akisisitiza kwamba bila uwekezaji endelevu hakuna kodi.

Dk. Mpango ameyasema hayo Februari 27, jijini Dar es Salaam alipomwakilishwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Jukwaa la Uwekezaji na Kodi 2024 lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa ya Julius Nyerere (JNCC) uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kufanya maboresho ya sera na kanuni ili kujibu changamoto za uwekezaji na wafanyabiashara ili waweze kulipa kodi kwa hiari na kuiwezesha Serikali kutekeleza mahitaji kwa Umma.

“Maoni haya yatatumika katika mchakato wa bajeti inayofuata bila uwekezaji hakuna kodi, Mawaziri wa Fedha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Sera, Mipango na Uwekezaji
zingatieni maoni ya sekta binafsi na walipa kodi, tuwe wanyenyekevu tuwasikilize walipa kodi na wawekezaji nakufanyia kazi mapendekezo yao ili tutengeneze vivutio vipya na kupata wawekezaji wapya nakutimiza lengo la kufikia kipato Cha kati mwaka 2025,” amesema Dk. Mpango.

Amesema jitihada hizo za Serikali ambayo imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi imepaisha makusanyo ya mapato yaliyotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na hiyo ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei uliofikia asilimia 3.2 kwa mwezi Julai hadi Desemba 2023 kiwango ambacho kipo ndani ya lengo la kati ya asilimia 3 hadi 7.

“Makusanyo ya shilingi Trilioni 22.6 kwa mwaka wa fedha 2022/23 yalipelekea kuongezwa kwa Bajeti kuu ya Serikali kutoka shilingi Trilioni 36 mwaka 2021/22 hadi Trilioni 44.4 mwaka 2023/24 ambazo zimesaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema.

Ametaja maendeleo hayo ikiwemo reli ya kisasa ya SGR ambayo imefanyiwa majaribio ya mafanikio, ukarabati wa miundombinu ya bahari na maziwa makuu, pamoja na asilimia 79 ya vijijini kufikiwa na huduma ya maji.

Aidha, amesema kuwa, Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya kuanzia ngazi ya Taifa hadi vituo vya afya kwa kuzingatia upatikanaji wa vifaa tiba, dawa pamoja na rasilimali watu huku katika sekta ya Elimu Rais Samia akiongeza wigo wa elimu bure hadi sekondari, miundombinu ya kufundishia na kujifunza, kutatua changamoto ya uhaba wa walimu.

Dk. Mpango amesema jukwaa hilo ni fursa kwa wadau kutoa maoni ya kodi na uwekezaji katika kuelekea bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2024/25.

“Mazuri yaliyotokana na jitihada za Serikali kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara zimeiweka Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji na kupelekea ukuaji wa uchumi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 5.0 mwaka 2023 huku matarajio ya ukuaji uchumi kwa mwaka 2024 yakiwa asilimia 5.5,” amesema.

Naye Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele katika masuala ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuweka mazingira wezeshi na katika sera za kodi serikali imekuwa ikielekeza kukusanya kodi kwa weledi, kutoa elimu, kusimamia sera ya ulipaji kodi na Usajili wa walipa kodi mpya.

Amesema ushirikishwaji huo utasaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo kulipa kodi kwa hiari pamoja na kutoa risiti kwa kila bidhaa inayonunuliwa huku changamoto ya kimfumo au mashine kuharibika ikiwa moja ya sababu ya ukwepaji ulipaji kodi kwa hiari.

Katika suala la ukadiliaji wa kodi Dk. Nchemba amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inakamilisha kujenga mfumo rasmi wa ukadiliaji huku ofisi ya msuluhishi wa masuala ya Kodi tayari imeanza kufanya kazi ya kutatua migogoro ya kikodi.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Sera, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kwa miaka mitano 2019/23 maboresho na mabadiliko 665 ya Sera, Sheria na kanuni za kodi na yasiyo ya kikodi yamefanyika na yote yamelenga kuboresha mazingira na kuvutia wawekezaji.

“Tanzania ina mvuto na mazingira mazuri ya uwekezaji na kupitia jukwaa hilo watapokea maoni mengi zaidi kwa lengo la kuvutia uwekezaji na ufanyaji biashara kwa wingi zaidi ili kodi itakayokusanywa iweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini,” amesema Profesa Kitila.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga amesema sekta binafsi nchini inatambua jitihada za Serikali katika kuboresha uchumi, kutambua mchango wa TPSF na kuitangaza nchi kimataifa kwa manufaa ya wananchi.

“Jukwaa hili limelenga kuimarisha ushirikiano baina ya Sekta za Umma na sekta binafsi katika kuboresha uchumi, kupokea maoni ya wadau na kujumuisha wadau katika maandalizi ya bajeti kuu ya Serikali na kueleza kuwa sekta binafsi inatambua jitihada za Serikali katika ukusanyaji wa kodi na TPSF imekuwa ikichangia asilimia 90 ya kodi inayokusanywa,” amesema Maganga.

Amesema, jukwaa hilo ni muhimu kwa wadau katika kuboresha uchumi wa nchi na kushauri TRA kukusanya kodi kwa kutumia weledi, kutoa elimu kwa wafanyabiashara ambao jukumu lao ni kuendelea kulipa kodi pamoja na Serikali kutanua wigo wa sehemu za makusanyo ya Kodi.

Ameishauri serikali kupitia mifumo na kuirahisisha sheria ya Kodi kwa wafanyabiashara wadogo pamoja na kuandika kwa lugha rahisi na TPSF itaendelea kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa hiari na kuweka msimamo wa kutotambulika kwa wafanyabiashara wasiolipa kodi katika vyama vyao.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu Mwamba alieleza kuwa jukwaa hilo limelenga kupata maoni ya wadau kuhusiana maboresho ya sera kodi kuelekea bajeti kuu ambayo pia itakasaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Jukwaa la Uwekezaji na Kodi kwa mwaka 2024 limebeba kauli mbiu ya ‘Maboresho ya Sera Katika Uwekezaji, Ukusanyaji Mapato ya Ndani na Ukuaji wa Uchumi Jumuishi” likiwa limeandaliwa na SJT na SMT kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles