26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango ataka nchi za Afrika kuja na mwarobaini wakuwezesha vijana

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango ametoa rai kwa washiriki wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kujadili namna bora ya kuwezesha rasilimali watu hasa vijana ili kuchochea ukuaji wa maendeleo na uchumi barani Afrika.

Dk. Mpango ametoa kauli hiyo leo Julai 25, jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha Kiufundi kilichowakutanisha mawaziri mbalimbali kutoka nchi za Afrika chenye lengo la kujadili mtaji wa rasilimali watu kilicho fanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) ambapo amesema nchi zinapaswa kutafuta namna bora ya kuboresha nguvu kazi ya vijani kwa sababu mafanikio ya maendeleo duniani kote yanategemea rasilimali watu.

Amesema uwekezaji katika elimu, afya na miundombinu utasaidia ukuaji wa sekta hizo.

“Nitoe rai yangu kwenu kikao hiki cha kiufundi nilichokifungua kijadiliane namna ya kupata rasilimali fedha ili kuweza kuendeleza rasilimali watu kwa kuhakikisha elimu inapatika, afya na miundombinu yote wezeshi itakayosaidia kukuza na kulea rasilimali watu,” amesema Dk. Mpango.

Amesema Serikali ya Tanzania imepiga hatua mbalimbali katika kuhakikisha inalinda na kukuza rasilimali watu kwa kuhakikisha inatoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, kuwekeza kwenye makundi maalumu na usawa wa jinsia.

Amesema katika kuboresha elimu wamewarudisha shuleni wasichana waliopata ujauzito wakiwa shule baada ya kujifungua huku Serikali ikiwa na lengo la kupitia sera ya elimu upya ili kutunga sheria itakayosaidia wanafunzi kujifunza kutokana na soko la ajira.

“Serikali ya Tanzania tumepiga hatua kubwa kwenye kuhakikisha tunalinda hizi rasilimali watu pamoja na kufanya elimu imfikie kila mtu, lakini pia kwenye sekta ya afya tumeboresha sana ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 67 hadi kufikia mwaka 2022,”amesema Dk. Mpango.

Amesema Serikali pia imewezesha huduma kwa kaya masikini ikiwamo upatikanaji wa huduma muhimu kila sehemu.

Aidha, amesema taarifa zinaonyesha Afrika bado inakabiliwa na changamoto ya rasilimali watu hivyo kikao hichp kinapaswa kuja na sera ambazo zitaboresha rasilimali watu.

Waziri wa Fedha

Awali, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwekeza kwenye rasilimali watu ni kuchochea maendeleo kwa taifa, hivyo Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo elimu na afya ili kuhakikisha rasilimali iliyopo inatunzwa.

Amesema mwaka 2017 Serikali ilitambulisha sera ya elimu bure kwa kwa shule za msingi na sekondari hatua ambayo imechochea ongezeko la asilimia 80 ya wanafunza waliojiandisha shule.

“Tanzania tumepiga hatua mbalimbali ili kulinda rasilimali watu katika sekta ya afya tumeweza kutoa mafunzo mbalimbali pamoja na kuajiri watu wenye ujuzi lakini tumejenga hospital kanda na rufaa 2,000, zahanati 700 na vituo vya Afya nchi nzima,” amesema Dk. Nchemba.

Amesema mkutano huo utakuwa kichocheo cha kubadilisha rasilimali watu na umekuwa msingi bora kwa watu, na umuhimu kuwapatia vijana ujuzi na kusisitiza ufundi stadi.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu kutoka nchi ya Cape Verde, Dk. Olavo Correia amesema ili kutatua changamoto ya rasilimali watu nchi za Afrika zinapaswa kujadili namna ya kupunguza umaskini kwenye nchi zao.

Amesema Afrika kuna vitu vingi vizuri ni bara lenye kila kitu na utajiri mwingi, hivyo maendeleo hufanywa na rasilimali watu.

“Bara letu lina watu wengi ni vijana lakini kumekuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na elimu, afya, ajira na miundombinu ili kuendeleza rasilimali watu lazima tubadilike na tupambane kuhakikisha hakuna rushwa, ufisadi, utakatishaji fedha,
” amesema Dk. Correia

Amesema Benki ya Dunia inashirikiana na nchi nyingi Afrika na inaongeza uwekezaji, viongozi wanapaswa kuendeleza ajenda hiyo ya rasilimali watu kwa Afrika ili kutengeneza mazingira ya kuishi kwa utu.

“Kuwekeza kwenye mtaji wa rasilimali watu ni muhumi kwasababu tutakuwa na rasmali watu wakajenga barabara,viwanja vya ndege na vitu vingine tutengeneze mabadiliko tusifanye mambo ya mazoea,” amesema.

Aidha, Dk. Correia amesema wanatarajia kuwa na mkutano mwaka 2024 nchini, Cape Verde wa kujadili jinsi ya kutokomeza umaskini uliokithiri na kwamba uwe ni utaratibu wa kila nchi kuandaa mkutano huo ili wahakikisha wanatokomeza umaskini uliokithiri Afrika.

Mkutano wa rasilimali watu unaoendelea jijini Dar es Salaam siku ya kesho Julai 26, unatarajia kukutanisha wakuu wa nchi kutoka nchi zote za Bara la Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles