25.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 28, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Kikwete: Bado kuna changamoto vifo vya watoto wachanga

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, amesema pamoja na Serikali kuwekeza vizuri katika sekta ya afya, bado kuna changamoto ya vifo vya watoto wachanga kwani imepungua kwa kiasi kidogo sana.

Amesema madaktari bingwa waliopo wanapaswa kuimarishwa ili kufika hadi ngazi za chini, pia kuboresha mfumo wa rufaa kwa wajawazito,watoto na kuweka mfumo mmoja wa gari la wagonjwa.

Amezungumza hayo jana Novemba 15,2023, jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa pili wa kisayansi kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto wenye kauli mbiu isemayo ‘Boresha Huduma ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto na Lishe kutokana na matokeo ya Kisayansi’.

Aidha ametaka wataalamu wa afya kupewa mafunzo ya mara kwa mara ili kuendana na wakati uliopo.

“Tusimamie kwa dhati mafunzo ya kazi ili kuhakikisha watoa huduma za afya wanaenda na wakati wapate ujuzi mpya wa maendeleo ya sayansi hii itasaidia hata waliosoma zamani waweze kuendana na wakati,”amesema Kikwete.

Amewataka wadau wa afya nchini pamoja na Serikali kuwekeza kwenye vyuo vya afya kwa kuangalia mitaala na njia zinazotumika kufundishia kwani zitakiwa kuendana na wakati uliopo.

“Katika eneo la afya tunapaswa tuwe na kauli mbiu ambayo itakua inawahamasisha kufanyakazi, nafikiri kauli mbiu hii ya ‘Tujiongeze Tuwavushe Salama’, hii itawapa hamasa ya kufanya kazi,” amesema.

Naye Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema nchi imepiga hatua katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai l00,000 mwaka 2015, mpaka vifo 104 kwa kila vizazi hai laki moja mwaka 2022.

Amesema mafanikio waliyoyapata yamechangiwa na mambo makubwa matatu ikiwemo wanawake kuwa na imani na vituo vya huduma ya afya.

“Maudhurio manne ya kliniki ya wajawazito yameongezeka kutoka asilimia 53 hadi asilimia 64 lakini idadi ya wanawake wanaojifungulia vituo vya afya imeongezeka kutoka asilimia 63 mwaka 2015 hadi asilimia 81,”amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Nasor Ahmed Mazlui, amesema serikali hizi mbili zikishirikiana zitafikia malengo ya kimataifa kabla ya kufika 2030.

“Tunapaswa wananchi na serikali kushirikiana ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea katika kupunguza vifo vya mama na watoto kwa kuwa nia tunayo basi mafanikio yatapatikana,”amesema Mazlui.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles