29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mwinyi awataka mawaziri kuimarisha haki za wanawake kiuchumi

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka mawaziri wa fedha na jinsia kwa nchi za Afrika kuboresha mipango ya maendeleo ili kuimarisha haki za kiuchumi za wanawake katika Bara zima.

Ameyasema hayo leo Novemba 15, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa Afrika wanaohusika na masuala ya fedha na jinsia kutoka nchi 22 wanachama wa Jukwaa la Usawa wa Jinsia (UN Woman) na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF_Afritac East).

Amesema mkutano huo umelenga kujadili namna ya kuwezesha wanawake na wasichana kiuchumi na kijamii kupitia ufadhili usawa wa jinsia.

“Kipengele cha jinsia kimejumuishwa kikamilifu katika mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano(2021/22-2025/26)na dira ya maendeleo ya Tanzania 2025 ambayo yote yanasisitiza dhamira ya nchi katika kukuza usawa wa jinsia katika kijamii,kiuchumi na kisiasa,”amesema Dk. Mwinyi.

Amesema sera zote za ubaguzi wa kijinsia zinapaswa kuondolewa na kutekeleza sheria, sera na kuweka mikakati ya uwekezaji ili kuwezesha upatikaji wa haki za wanawake na wasichana.

Dk. Mwinyi ameongeza kuwa mabadilko ya tamaduni yanapaswa kuingiliwa ili kubadilisha kanuni za kijamii zinazoleta au kuchochea ubaguzi.

Amesema Tanzania imepiga hatua katika kuongeza upatikanaji wa huduma fedha kwa wanawake kwani kumekuwa na ongezeko kubwa la wanawake wenye kutumia huduma za kibenki kutoka asilimia 66 mwaka 2017 hadi asilimia 80 mwaka 2023.

“Mafanikio haya ya ushirikishwaji wa kifedha kwa wanawake ni matokeo ya kuongezeka kwa utoaji wa namba ya vitambulisho vya taifa kwa wanawake na bidhaa za kifedha sasa zinafikiwa na wanawake,”amesema.

Amesema kuwa mustakabali wa Afrika kuna uwezekano mkubwa wakutokufikiwa ikiwa wanawake na wasichana wataachwa nyuma.

Ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania imejitolea kushughulikia usawa wa kijinsia kwa vitendo katika nyanja zote za mwanamke.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu Dk. Dorothy Gwajima, amesema kuna haja kubwa ya kuwekeza kwenye jinsia ili kuisaidia serikali kutotumia fedha nyingi kwenye mapambano ya jinsia badala yake fedha hizo zipelekwe kwenye mahitaji ya kijamii.

Amesema viongozi hao watajadili namna bora ya kushughulikia athari za mapungufu ya jinsia katika uchumi kwa ujumla na kuchochea ufadhili wa masuala ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kupitia bajeti zao ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

“Kwa kuacha hizi tabia kandamizi zitasaidia hizi fedha tunazotumia katika kupambana na ukatili zikaongezwa kwenye maendeleo na suala la ukatili si suala la Tanzania tu ni la Bara zima,” amesema Dk.Doroth.

Amesema masuala ya ukatili wa kijinsia yanayofanywa kutokana na mila na desturi yanarudisha nyuma maendeleo ya wanawake ambao wanamchango mkubwa kwenye maendeleo ya sekta zote.

Aidha amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kupiga hatua katika kuendeleza na kuwekeza kwenye masuala ya kijinsia kwani sasa hivi idadi kubwa ya viongozi nafasi ya mwanamke ipo na inafanya vizuri.

Naye Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwekeza kwa wanawake ni kichocheo kikubwa cha uchumi katika nchi, hivyo serikali itaendelea kuwawezesha na kutunga sera zitakazosimamia mipango na maendeleo endelevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki UN Women, Dk.Maxime Houinato amesema mawaziri wa fedha wanahitajika ili kuangalia namna bora ya kuwawezesha wanawake.

Aidha ametoa rai kwa serikali na sekta binafsi kuhakikisha mabinti wanapotoka chuo wasaidiwe kupata kazi ili kuepuka kuingia kwenye ukatili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles