Veronica Romwald na Nicodemas Kikwati (GHITBS), Dar es Salaam
MKURUGENZI wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba, amefanyiwa upasuaji wa mguu wa kushoto.
Upasuaji huo umefanyika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI).
Akizungumza na MTANZANIA jana hospitalini hapo, Dk. Bisimba alisema alifanyiwa upasuaji huo juzi jioni na anaendelea vizuri na matibabu.
“Namshukuru Mungu naendelea vizuri, nimefanyiwa upasuaji na madaktari wameniwekea vyuma kuisaidia mifupa yangu iweze kujishika, naamini nitapona,” alisema.
Alisema ipo haja kwa jamii hususan madereva kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani kwa sababu ajali nyingi zinaweza kuepukika.
“Kwa kweli nilishangaa kupata ajali Dar es Salaam tena Jumapili siku ambayo magari huwa si mengi mjini wakati nilitoka na gari lile Mlimba (Morogoro).
“Ajali ile ilitokea kwa sababu dereva aliyetugonga hakuwa makini, alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi.
“Pale tulikuwa kwenye makutano ya barabara na taa zilituruhusu, gari ya mbele yetu ilipita na sisi tulipotaka kupita ndipo alipotugonga,” alisema.
Dk. Bisimba alisema alifarijika alipotembelewa na Rais Dk. John Magufuli katika Hospitali ya Agha Khan ambako alikuwa amelazwa awali.
Dk. Bisimba alipata ajali Novemba 8 mwaka huu kwenye taa za Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.