28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Jingu ataka sheria kusimamia watoto wa mtaani

Na Ramadhan Hassan,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dk. John Jingu amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutunga Sheria ndogo kwa ajili ya kusimamia afua za kudhibiti suala la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani pamoja na ombaomba.


Akizungumza leo Septemba 13,2021,Jijini Dodoma wakati akizungumza  katika kikao cha kujadili na kuweka mikakati ya kushughulikia tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani,Katibu Mkuu huyo amesema bado suala la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ni tatizo.


Kikao hicho kiliwakutanisha Makatibu Tawala wa Mikoa yote nchini,Makamanda wa Polisi wa Mikoa yote nchini na Makamanda wa Kanda Maalum za Kipolisi,Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.


“Pia,kufanya zoezi la utambuzi wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na omba omba katika mikoa yote pamoja na kuhakikisha kuwa watoto hawa wanarejeshwa katika jamii zao.Kutoa elimu kwa jamii ili waepukane na kutoa fedha kwa ombaomba kwa vile inahamasisha ombaomba wakiwemo watoto kuwepo mitaani.


“Tafiti mbalimbali zimefanyika ili kubaini hali halisi ya watoto hawa mathalani “Head Count Survery” ya mwaka 2017 katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya, Iringa na Dar es salaam ilibaini jumla ya watoto 6,393 ambao walikuwa wanaishi na kufanya kazi mtaani. Zaidi ya asilimia 90 ya watoto hao wazazi/walezi wao wanafahamika wanapoishi,”,”amesema Dk. Jingu.


Amesema pamoja na jitihada hizi ambazo zimekwisha kufanyika  bado changamoto ya  watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani pamoja na ombaomba  ni kubwa.


“Kwa msingi huu tumeona ni vyema kuwa na kikao hiki chenye wadau hawa muhimu ili tuweze kujadili na kuwa na mkakati wa pamoja unaolenga kuondoa changamoto hii,”amesema.


Amesema kikao hicho  ni muhimu  kwani kitasaidia kujadili na kuwa na mkakati wa  pamoja wa  namna bora ya kuondokana na changamoto hiyo.


“Lengo kuu la kuwa na mkakati wa pamoja ni kuwa na mtizamo wa pamoja unao unganisha  nguvu zetu hali tukidhamiria  kumaliza tatizo hili kwa pamoja kama sio kulipunguza.Kwa mantiki hii, ni mategemeo yangu kuwa kwa mchanganyiko huu wa washiriki tuliohudhuria kikao hiki, tutatoka na mikakati inayotekelezeka ya kumaliza tatizo hili,”amesema.


Naye,Kaimu Kamishna Ustawi wa Jamii, Shilungu Ndaki amesema tatizo la  watoto wanaoishi mitaani na kufanya kazi mitaani bado ni kubwa ambapo amedai lengo la kikao hicho ni kuweka mikakati ya pamoja na kuja na suluhisho la jinsi ya kuondoa tatizo hilo.


Ndaki amesema tayari watoto 1506, wamerejeshwa kwenye familia zao kutoka mikoa ya Dar, Mwanza, Arusha, Mbeya na Iringa licha ya kuwa suala la watoto kuishi mitaani ni changamoto.


Akiwasilisha mada iliyohusu jitihada za Serikali katika kutatua changamoto  wanazokutana nazo watoto wa mitaani na wanaofanya kazi mitaani,Ndaki amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuwasaidia watoto wanaioshi mitaani ikiwemo kuwapeleka shule ili waweze kupata elimu.


Kwa upande wake, Mkurugenzi mkaazi wa Shirika la PACT Tanzania, Mariana Balampama amesema tayari wamewafikia watoto 8300  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo amedai pia  kwa kushirikiana na Serikali wameweza kutekeleza miradi mbalimbali.


Mkurugenzi huyo ameitaka jamii kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha watoto hao wasitoke mashuleni na kwenda mitaani.


“Napenda kuishukuru Serikali kwa kutupa miongozo ambayo imekuwa ikitusaidia,tunaahisi kuendelea kushirikiana nayo kuhakikisha watoto wanakuwa salama,wanakuwa na afya njema kikubwa tumejifunza suluhisho la watoto wa mitaani  linahitaji mambo mengi,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles