Na CLARA MATIMO -MWANZA
WAKATI Taifa limeadhimisha kumbukizi ya miaka 21 tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere afariki, waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza wamekutana na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Butiama wa kwanza ambako muasisi huyo wa Taifa alizaliwa, Dk Angeline Mabula, ambaye amesema maisha yake yalikuwa ya tofauti.
Dk Angelina ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema maisha aliyoishi mwalimu Nyerere hayakuwa yakiendana kabisa na wadhifa wake kwa sababu alikuwa ni kiongozi anayeshirikiana na wana kijiji wenzake kila alipoenda likizo.
Dk Angelina aliyasema hayo jana jijini hapa alipozungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza kwenye mkutano uliolenga kuwapa historia ya Wilaya aliyozaliwa Mwalimu Nyerere akiwa kiongozi wa kwanza wa eneo hilo.
Alisema tabia hiyo kwake imekuwa ni fundisho kwamba unapokuwa na madaraka inatakiwa uishi maisha ambayo umekuwa ukiyaishi kabla ya kupata wadhifa huo.
“Ukiishi hivyo jamii itatambua kwamba uko nayo pamoja lakini unapokuwa na wadhifa halafu unajiona wewe uko juu kuliko wengine hauwezi kabisa kuacha alama yoyote kwa wengine baada ya kuondoka, unaposhirikiana na wenzako mtajenga umoja ambao utakuwa ni chachu kwa maendeleo ya taifa na watu unaowaongoza.
“Baba wa Taifa alisema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, ukishirikiana na jamii itasaidia kujengeana uwezo wa kujitegemea katika maisha badala ya kutegemea misaada kutoka nje ya nchi ambayo ingeweza kutudumaza zaidi kiuchumi,” alisema.
Dk Angelina alisema anajivunia kubadili sura ya maadhimisho ya siku ya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kutoka kwenye hadhi ya kifamilia hadi kitaifa.
Alisema mwaka 2012 baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Butiama alikuta wakiadhimisha siku hiyo kifamilia akaona eneo lile limepewa hadhi ya wilaya na tukio hilo ni kubwa linahadhi ya kitaifa, taifa lilikuwa linaadhimishwa sambamba na hitimisho la mbio za mwenge aliongea na wanafamilia wakakubaliana kuipandisha hadhi siku hiyo.
“Tulianza kuadhimisha siku hii kwa kuita viongozi wa umoja wa wazee kutoka nchi nzima lakini kila mwaka tulikuwa tukialika wageni rasmi tofauti tofauti vijana nao wakawa wanafanya kongamano kwa hiyo tukawa na matukio mawili kwa wakati mmoja.
“Wazee walipata fursa ya kuwaeleza vijana maisha ya Baba wa Taifa na namna ambavyo taifa lilianza mchakato wa kupata uhuru wakiongozwa na baba wa taifa vijana wengi walifaidika na elimu ya kujua historia ya muasisi wa taifa lao kutoka kwa wazee ambao walifanya naye kazi,” alisema.
Alisema vijana walipata fursa ya kuingia ndani ya jumba la makumbusho ya Baba wa Taifa ambalo lina zana na vifaa alivyovitumia enzi za uhai wake lenye historia nzima ya maisha yake kitendo hicho kiliwasaidia kujua jinsi alivyoishi na falsafa zake za elimu ya ujamaa na kujitegemea.
Kwa mujibu wa Dk Angelina, wakazi wa Wilaya ya Butiama walikuwa wamezoea kuishi kwa kufuata na kuongozwa na mila za kitemi hivyo alivyoenda kuanza kazi baadhi ya watu walimpokea kwa mtazamo hasi wakihofia kama ataweza kuwaongoza bila kuzivunja.
Alisema alishirikiana na wazee pamoja na mjane wa Baba wa Taifa mama Maria Nyerere ambao walielekezana mila nzuri zikafuatwa na kandamizi walishauriana wakaziondoa.
“Ukweli unajua sehemu ambayo inautawala wa kichief mara nyingi kuna mfumo dume hata mimi nilipoteuliwa nilikutana na changamoto hizo kuna wakati kulikuwa na migogoro ya shule viongozi wote wa ngazi za juu tulikuwa wanawake, akiwemo Katibu wa CCM , Mkurugenzi na Mwanasheria tulipofika eneo lile kwa ajili ya kutatua mgogoro huo baba mmoja alisema ‘hapa sioni kama tutapata muafaka kwa sababu meza yote pale mbele viongozi ni wanawake’,”alisema.
Alisema baadhi ya wazazi walikuwa wakigoma kuwalipia ada watoto wao wa kike ikamlazimu kuwaweka rumande matendo hayo yote ni viashiria vya mafumo dume lakini aliwaelimisha wakaelewa, hadi anaondoka wilayani humo hakuna aliyependa aondoke kwa sababu alikuwa akikaa nao kwenye vikao vya kushauriana ananukuu maneno ya Baba wa Taifa.