32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. 30 za sekeseke la Ukawa bungeni

UPINZANI KUONDOKA-4*Zomea zomea yao yawatia joto viongozi

*Waimba Maalim Seif…Maalim Seif…Maalim Seif

NA MAREGESI PAUL, DODOMA

WABUNGE wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana walichafua hali ya hewa bungeni baada ya kuwazomea baadhi ya viongozi walioongozana na Rais Dk. John Magufuli kwa ajili ya shughuli ya uzinduzi wa Bunge la 11.

Tukio hilo la kwanza katika Bunge hilo lililoanza Novemba 17, mwaka huu na kuahirishwa jana hadi Januari 26 mwaka 2016, lilianza jana saa 9:35, zikiwa ni dakika chache tu kabla Rais Magufuli hajatoa hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge.

Dalili za wabunge hao kufanya vurugu zilianza saa 9:16, baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, kutengua kanuni za Bunge ili kuwawezesha wageni wasiokuwa wabunge kuingia bungeni na kukaa eneo maalumu lililotengwa kwa ajili yao.

Wakati akitengua kanuni hizo, Masaju alizitaja kanuni za 139 (1) na 143 (f), kwamba ndizo zinazohusika katika suala hilo kwa kuwa ujio wa Rais Magufuli ulihusisha baadhi ya wageni wasiokuwa wabunge.

Aliwataja wageni hao kuwa ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Serikali hiyo, Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.

Baada ya hatua hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisimama na kuomba mwongozo kwa Naibu Spika, Dk. Tulia Akson, akitumia kanuni ya 68 (7) inayoruhusu mbunge kusimama na kuomba mwongozo juu ya jambo lililozungumzwa muda mfupi bungeni.

Katika mwongozo wake, Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alitaka kujua ni kwanini kati ya wageni waliotajwa kwa ajili ya kuingia bungeni, yumo Dk. Shein, Seif Idd na Kificho wakati hawastahili kuwapo?

Kwa mujibu wa Lissu, viongozi hao watatu hawakustahili kuingia bungeni kwa kuwa muda wao wa kukaa madarakani umekwisha kwa mujibu wa Katiba.

“Mheshimiwa Naibu Spika, naomba utupatie mwongozo wako juu ya ujio wa Dk. Shein, Seif Idd na Kificho kwa kuwa muda wao wa kukaa madarakni umekwisha tayari.

“Kwa hali ilivyo leo, hatuna rais halali wa Zanzibar, hatuna makamu wa kwanza na wa pili halali wa Zanzibar na pia hatuna Spika halali wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

“Kwa mujibu wa ibara ya 28 (2) ya Katiba ya nchi, muda wa miaka mitano ya Serikali ya Zanzibar umekwisha tangu tarehe 2 mwezi huu, kwani ndipo miaka mitano ilipokoma.

“Kwa hiyo, mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwongozo wako kwa sababu nataka kujua kama jambo hili linaruhusiwa,” alisema Lissu.

Baada ya kusema hayo, mbunge huyo alikaa na Naibu Spika alisimama na kusema ibara hiyo kifungu cha kwanza, kinasema madaraka ya Rais wa Zanzibar yatakoma baada ya rais mwingine kuapishwa.

“Mheshimiwa Lissu, ibara hiyo hiyo uliyosoma, ukiisoma katika sehemu ya kwanza, inasema Rais wa Zanzibar ataendelea kuwa rais hadi hapo rais anayefuata ale kiapo cha kuwa rais na hadi sasa hakuna rais aliyeapa Zanzibar,” alisema Dk. Tulia na kushangiliwa na wabunge wa CCM.

Hatua hiyo ilipokoma, ofisa wa Bunge alitoa maelekezo ya jinsi wageni watakavyoingia ukumbini na jinsi watakavyokuwa wakisindikizwa.

Ilipotimu saa 9:35, Kificho aliingia ukumbini na wabunge hao wa upinzani walianza kumzomea huku wabunge wa CCM wakimpigia makofi ya kumkaribisha.

Dakika moja baadaye, Balozi Idd naye aliingia ukumbini ambapo wabunge hao wa upinzani walimzomea, lakini yeye aliwapungia mkono huku akitabasamu.

Ilipotimia saa 9:40, Dk. Shein akiwa katikati ya maaskari wa Bunge waliokuwa wamevalia majoho aliingia na wakati huo wapinzani walianza kutaja jina la aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Wakati wabunge hao wakiendelea kulitaja jina hilo kwa staili ya kuimba wakisema; Maalim Seif…Maalim Seif… Maalim Seif…, kundi la askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliingia ukumbini na kusimama pande mbili za ukumbi huo.

Saa 9:44, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliingia ukumbini akiwa na ulinzi unaofanana na ule wa Shein.

Samia aliongozana na Naibu Spika, huku kelele za wapinzani waliokuwa wamesimama, zikiendelea.

Baada ya dakika moja tangu Makamu wa Rais alipoingia, Rais Magufuli aliingia akiongozwa na Spika Ndugai na kuelekea katika eneo lake maalumu la kukaa, huku kelele za wapinzani zikiendelea kushika kasi.

Kelele hizo zilimfanya Spika Ndugai ahamaki na kusimama akiwa katika kiti chake na kuwataka wabunge hao wa upinzani wasiendelee kupiga kelele ili Bunge liendelee.

“Waheshimiwa wabunge, naomba mkae chini, waheshimiwa wabunge nawaomba mkae chini kwa mara ya kwanza. Kwa mara ya pili nawaomba waheshimiwa wabunge mkae chini,” alisema Spika Ndugai lakini hakusikilizwa.

“Waheshimiwa wote mnaofanya fujo nawaomba tokeni nje kwa hiari yenu, nawaomba mtoke nje haraka,” alifoka Spika.

Baada ya maagizo hayo, wabunge hao walianza kukusanya mizigo yao mmoja baada ya mwingine na kuondoka ukumbini huku wakizomewa na wabunge wa CCM.

Wakati hayo yote yakitokea, marais wastaafu waliohudhuria tukio hilo, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete nyakati fulani walionekana kutabasamu, tofauti na Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amani Abeid Karume, ambao muda wote walionekana wakiwa hawatabasamu wala kucheka.

 

 

  1. MAGUFULI

Akizungumzia tukio hilo katika hotuba yake ya kulifungua rasmi Bunge, Rais Magufuli alisema ni la aibu na kwamba wabunge wanatakiwa kuachana na tabia hiyo kwa kuwa wananchi wanahitaji maendeleo na wala hawahitaji mivutano, mipasho na vijembe bungeni.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, baada ya miaka mitano, wabunge na yeye mwenyewe watapimwa na wananchi kwa jinsi walivyofanya maendeleo na kwamba hawatapimwa kwa vurugu na vijembe walivyovitoa wakiwa bungeni.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli alimpongeza Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ambaye hakushiriki vurugu hizo na hakutoka nje.

Kwa upande wake, Spika Ndugai alimuomba radhi Rais Magufuli kwa kilichofanywa na wapinzani na kuwataka wasirudie kitendo hicho.

“Nakuomba radhi sana Mheshimiwa Rais, lakini pia waheshimiwa wabunge mnao uwezo wa kunifanya niwe Spika mwema au niwe Spika mbaya.

“Kilichotokea leo uwe mwisho na leo nimeshindwa kuchukua hatua kwa sababu kuna wazee hawa, lakini siku nyingine hawatakuwapo, sipendi kuongea sana, iishie hapo,” alisema Spika Ndugai.

Uwepo wa vurugu hizo ulitarajiwa, kwa kuwa mwanzoni mwa wiki, viongozi wakuu wa Ukawa walizungumza na waandishi wa habari mjini hapa na kueleza nia yao ya kuwazuia Dk. Shein na wenzake hao kuingia bungeni kwa kuwa si viongozi halali.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles