26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli – Nitapasua majipu

IMG_0209Agatha Charles na Aziza Masoud

RAIS John Magufuli jana alilizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano kwa kurejea mambo aliyoyaahidi wakati wa kampeni zake za urais huku akijipa jukumu jipya aliloliita la kupasua majipu.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge hilo iliyochukua muda wa masaa mawili, Rais Magufuli alisisitiza kuwa amejipa kazi ya kupasua majipu yanayoitesa serikali ili kuijenga upya Tanzania na kurejesha matumaini yaliyopotea ya Watanzania.

Hotuba hiyo ambayo ni ya kwanza kuitoa tangu alipochaguliwa na kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, pamoja na mambo mengine ilibeba merejeo na ahadi za kampeni, mgogoro wa uchaguzi Zanzibar, vipaumbele vya serikali kwa kipindi cha miaka mitano, Katiba Mpya pamoja na ushirikiano wa Kimataifa na nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumzia marejeo ya ahadi alizozitoa wakati wa kampeni zake za kuwania urais, alisema hakutoa ahadi ili aweze kupigiwa kura, bali aliyoyaahidi atayatekeleza.

“Niwahakikishie wananchi mambo yote tuliyoyaahidi tutayatekeleza, tuliyoahidi tuliahidi na ahadi ni deni. Nawahakikishia wananchi sikutoa ahadi ili nipigiwe kura, bali niliyoyaahidi nitayatekeleza,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wakati wa kampeni alibaini kuwa maeneo mengi yana tatizo la rushwa, huku Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikilegea kusimamia upotevu wa mapato, kukusanya kodi, wizi, uzembe.

Tanesco

Rais Magufuli alilitaja Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuwa limekithiri kwa ubabaishaji unaosababisha kuwepo kwa tatizo sugu la mgawo wa umeme.

“Kila siku Mtera wanafungulia maji usiku halafu wanasema hayatoshi, ikifika usiku wanawapa wa majenereta, tuta’deal’ nao, nami nawaambia nitadeal nao kweli kweli.

“Tutasimamia hujuma zote za kuzima umeme ili wafanyabiashara wauze majenereta,” alisema Magufuli.

 

Huduma za afya

Rais Magufuli alirejea ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni kuwa kila kijiji kitakuwa na zahanati, wilaya zitakuwa na hospitali na mikoa yote itakuwa na hospitali za rufaa.

“Lengo ni watu kutibiwa hapa na kutopelekwa nje ya nchi, imekuwa kawaida hata watu wakiugua mafua kwenda nje ya nchi wakati hapa kuna wataalamu,” alisema Magufuli.

Elimu

Akizungumzia sekta ya elimu, Rais Magufuli alisema inakabiliwa na uhaba wa vifaa, michango, malalamiko ya walimu yasiyokwisha, ukosefu wa nyumba za walimu na ukosefu wa  madawati kwa wanafunzi.

Alisema ahadi yake ya elimu ni bure alimaanisha kuwa kuanzia Januari hakuna mwanafunzi atakayetozwa kiasi chochote cha fedha kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

Polisi

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, Dk. Magufuli alisema kuna malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, madai ya askari, vifaa, Zimamoto kuchelewa kufika kwenye tukio au kukosa maji.

 

Kilimo

Akizungumzia sekta ya kilimo, alisema inakabiliwa na uhaba wa maghala, wakulima kukopwa mazao, ukosefu wa wataalamu wa kilimo huku sekta ya uvuvi ikiongozwa na uvuvi haramu na uwekezaji mdogo.

“Tutatilia mkazo kwa kuangalia kwa mtazamo wa kibiashara kwa kuwa na viwanda vya kisasa vitokanavyo na kilimo, ufugaji na uvuvi.

“Hapa wanatumia zana duni, lakini tunazalisha kwa asilimia 95 na inaonyesha mchango wake ni mkubwa na nawapongeza kwa mchango wao. Nawaahidi wakulima, wafugaji na uvuvi sitawaangusha,” alisema Magufuli.

Alisema wakulima na wavuvi ni maskini na mapato yao yako chini hivyo inapaswa kuboreshwa kwa sekta hizo na kusababisha vijana wengi kushawishika kuingia.

“Tuliahidi kuwapatia pembejeo kwa kuwapa zana za kisasa na wataalamu wa ugani na uhakika wa soko, kuondoa ushuru mbalimbali, kukopeshwa na benki ya kilimo,” alisema Magufuli.

Muungano

Rais Magufuli alisema serikali yake itashughulikia masuala mbalimbali, ikiwemo kuimarisha muungano kwa kushughulikia pia suala la mgogoro wa kufutwa matokeo ya Uchaguzi Zanzibar.

“Nilipoapa kuwa rais niliapa kuulinda, hata bila kiapo mimi ni muumini wa Muungano bora kabisa wa hiari, tena uliosainiwa kwa kalamu si kwa mtutu na waasisi wetu.

“Naamini Muungano na ndio salama yetu, hivyo kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar na Chama cha Wananchi (CUF) naomba Mungu atujalie tulimalize salama na Samia (Makamu wa Rais Samia Suluhu) ana uzoefu wa masuala ya Muungano kutokana na kufanya kazi katika Wizara inayoshughulikia masuala ya Muungano.

“Na mimi na Dk. Shein (Rais wa Zanzibar Ali Mohamed Shein) tutashughulikia hilo,” alisema Magufuli.

 

Katiba mpya

Kuhusu Katiba mpya, Rais Magufuli alisema Serikali yake imepokea kiporo cha katiba.

“Serikali yangu imepokea kiporo, nawahakikishia kwamba tunathamini hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kwa Katiba mpya. Tunathamini Bunge Maalumu lililotupatia Katiba pendekezwa, tutaendelea ili ipatikane,” alisema Rais Magufuli.

Rushwa na ufisadi

Akizungumizia suala  la rushwa na ufisadi, Rais Magufuli alisema  wananchi wamechoshwa na rushwa  na vitendo vya ufisadi vinavyoendelea nchini na kuahidi kuvishughulikia.

“Wakati naomba kura na na kuzungumzia rushwa na ufisadi sikufanya hivyo kuwarubuni wananchi, niliongea kwa dhati kabisa kwa sababu wananchi wanachukia na wamechoshwa  na mimi pia nachukia na chama changu ipo kwenye ilani, lakini sina uhakika kama hakitoi na kupokea rushwa,” alisema Dk. Magufuli.

Muundo wa Serikali

Akizungumzia kuhusu muundo wa serikali, Dk. Magufuli alisema anataka serikali ndogo ambayo itajikita katika kuwahudumia wananchi na si kuwasumbua.

“Sitaki watendaji ambao watawazungusha wananchi, nataka serikali ndogo ya wachapakazi, natoa rai kwa watumishi wazembe wajiandae, tumewavumilia vya kutosha, wametuchezea vya kutosha, wametuchakachua vya kutosha  hivyo vyote muda wake umekwisha, lugha tupo kwenye mchakato tunaendelea na ufuatiliaji hakuna tena, hatuwezi kuwa na watu wanaolipwa mishahara bila kufanya kazi,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema ili kuhakikisha kunakuwa na ufanisi, serikali itaendelea kuboresha mishahara na mazingira ya kufanyia kazi, kufanya jitihada za kupunguza kodi ya wafanyakazi (PAYE)  pamoja  na kutoa motisha kwa wafanyakazi.

Alisema serikali pia itaongeza mshahara wa wafanyakazi kadri uchumi utakavyokuwa unapanda.

Mapato na matumizi

Akizungumzia suala la mapato na matumizi, Dk. Magufuli alisema  ndani ya miaka mitano watahakikisha kila mmoja anayestaili  kulipa kodi analipa na kuwachukulia hatua wakwepaji wa kodi.

“Kila mwananchi ahakikishe anadai risiti ukinunua bidhaa, kila senti inayopatikana itaelekezwa katika kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Dk. Magufuli.

Safari za nje

Dk. Magufuli alisema kuwa ili kuendelea kudhibiti matumizi ya serikali, aliamua kusitisha safari za nje kwa watumishi na kiongozi yeyote atasafiri kwa sababu maalumu, tofauti na hapo kazi zinazohitajika kufanywa katika nchi hizo zitafanywa na mabalozi husika.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2013 mpaka 2015, Sh bilioni 356.324 zilitumika kwa safari za nje, kati ya hizo tiketi za ndege ziligharimu Sh bilioni 183.17, posho za ……………….zimetumika  Sh bilioni 104.552, mafunzo ya nje Sh bilioni 68.62.

“Wizara zilizoongoza kusafiri nje ya nchi zimeongozwa na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Ukaguzi,” alisema Dk. Magufuli.

Mbali na Wizara ya Mambo ya Nje kushika namba mbili kwa kusafiri nje ya nchi, hivi karibuni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe, alikaririwa akisifia uamuzi wa rais kufuta safari za nje na kudai kuwa walikuwa wakigongana angani kama nyumbani kuna moto.

Rais Magufuli alisema kuwa fedha za nje zingeweza kufanya vitu mbalimbali, ikiwemo kujenga barabara ya kilomita 400 za lami pamoja na kutengeneza madawati.

“Tunapodhibiti safari za nje wabunge naomba mtuelewe na mtuunge mkono, safari za mafunzo tutaangalia utaratibu kuliko kundi kubwa kwenda huko, bora mwalimu aje huku kuwafundisha kwa suala la kikazi litashughulikiwa na balozi aliyeko huko kama kutakuwa na ulazima wa kwenda kiongozi basi tutahakikisha haendi na msafara wa watu wengi.

Kuna watu hapa wanafanya mambo ya ajabu na aibu, watu wanakwenda kukaa vikao vya bodi nje ya nchi  wakati wananchi wana shida, kweli hii sawa, bora niseme ukweli kwa sababu sitaki kuwa mnafki, wapo watu wamesafiri nje mara nyingi kuliko safari ya kwenda kuwasalimia mama zao,” alisema Rais Magufuli.

Alisema  haoni sababu za watu kuendelea kufanya mikutano hotelini wakati wizara zina kumbi na kuna mikutano ambayo inaweza kufanyika hata chini ya miti.

Aliongeza kuwa serikali yake pia itapunguza warsha na makongamano kwakuwa yanakula fedha nyingi na kuongeza matumizi wizarani wakati hazileti tija katika utendaji kazi.

Rais Magufuli pia aliwataka wabunge kurekebisha sheria ya manunuzi kwakuwa ni mbaya  kwa matumizi ya serikali.

“Hii sheria ya manunuzi naomba wabunge tusaidiane tuirekebishe, kuna watu wananunua kalamu ya Sh 1,000 kwa Sh 10,000, hii sheria ni mbaya haifai,” alisema Rais Magufuli.

Alisema atasimamia ukiukwaji wa maagizo na maelekezo kwa kuhakikisha samani zote za maofisini ziwe zinatoka za ndani pamoja na manunuzi ya magari.

“Tutadhibiti ununuzi wa magari ya gharama, mfano injinia badala ya Pick up unaenda kununua V8, unaenda kukagua miradi ya nini  sasa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema atachunguza na kudhibiti matumizi ya serikali kwa kuzingatia vipaumbele vya kupunguza urasimu, kubana matumizi, kurejesha nidhamu ya kazi serikalini.

Alitaja vipaumbele vingine ni kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, kuondoa mianya ya ukwepaji kodi, kuweka nidhamu ya matumizi ya serikali pamoja na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima.

Aidha Rais Magufuli aliwataka Watanzania kufanya kazi na kuacha kupoteza muda mwingi vijiweni.

Mambo ya Nje

Akizungumzia kuhusu mahusiano na nchi za nje, alisema serikali yake itaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali na kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Tutaendelea kuwa waumini, wanachama waaminifu wa Jumuiya za Nchi ya Maendeleo ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC),” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles