30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto ageuka

zitto00Evans Magege na Jonas Mushi

MBUNGE wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, jana hakutoka bungeni wakati wabunge wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walipoamriwa kufanya hivyo na Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya kukataa kuacha kuzomea na kupiga kelele kwa minajili ya kumzuia Rais John Magufuli kuzindua Bunge la 11.

Awali Zitto alionekana kuungana na Ukawa kabla Rais Magufuli hajaingia ndani ya Bunge.

Tukio ambalo lilionekana kuwaunganisha Zitto na Ukawa ni lile la kukataa kusimama wakati viongozi wakiwa wanaingia ndani ya Bunge hilo.

Wakati wenzao wa CCM wamesimama, Zitto pamoja na wabunge wa Ukawa walikuwa wamekaa lakini wakati wabunge hao wanaimba na kuzomea yeye alionekana akiwa ametulia.

Watu wanaomfuatilia Zitto wanasema hii si mara ya kwanza kwake kufanya hivyo, kwani mwaka 2010 wakati wabunge wa upinzani hususani Chadema na CUF walipotoka bungeni na kususia hotuba ya uzinduzi wa Rais Jakaya Kikwete kwa madai kutotambua uchaguzi uliomrejesha madarakani, mwanasiasa huyo hakutokea kabisa bungeni.

Wakati hayo yakitokea, kulikuwa na maneno yaliyokuwa yakiendelea chini kwa chini kuwa Zitto alikuwa hakubaliani na uamuzi wa wenzake wa kususia hotuba ya Rais Kikwete na ili kukwepa lawama aliamua kutotokea bungeni.

Katika tukio la jana baadhi wanaona ni kama vile Zitto ameigeuka kauli yake ya kutomtambua  Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein, kutokana na kitendo chake hicho cha kuendelea kubaki bungeni na hata kusikiliza hotuba ya ufunguzi wa Bunge iliyotolewa na Rais John Magufuli.

Zitto ambaye alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema misingi ya Katiba inaonyesha kuwa baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kwa upande wa Zanzibar kufutwa na Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC), visiwa hivyo havina Serikali na kwa mantiki hiyo mtu kuitwa rais ni sawa na uhaini.

“Mpaka leo ninapozungumza, kikatiba Zanzibar hakuna Serikali …na yeyote anayeitwa rais wa Zanzibar kikatiba amepindua, katika hali ya kawaida anapaswa kushtakiwa kwa uhaini na kosa la uhaini adhabu yake ni kifo,” alikaririwa Zitto.

Katika muktadha huo kitendo cha wabunge wote wa upinzani ambao wako chini ya mwavuli wa Ukawa kutoka nje ya Bunge na kumuacha Zitto pekee bungeni akiungana na wabunge wa CCM kusikiliza hotuba ya Rais Magufuli kama ilivyowahi kufanywa na wabunge wapinzani wa aina ya Augustine Mrema na John Cheyo, kimetafsiriwa kwamba mwanasiasa huyo amegeuka kauli yake ya awali.

Akizungumzia tukio la zomea zomea na kutoka nje kwa wabunge wa Ukawa, Zitto alisema jambo hilo ni changamoto ya kidemokrasia.

Hata hivyo, katika maelezo yake hayo  aliyoyatoa wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji nchini (TBC), hakugusia suala la viongozi wa Zanzibar.

Zitto ni mbunge pekee wa chama cha upinzani ambacho hakina ushirikiano na vyama vinavyounda Ukawa.

Mwanasiasa huyo chini ya chama chake cha ACT- Wazalendo amewahi kuomba ushirika wa Ukawa lakini viongozi wa umoja huo walimkatalia wakimuhofia kutumika na baadhi ya viongozi wa Serikali.

Zitto aliamua kujiunga na chama cha ACT- Wazalendo mwaka huu baada ya kesi ya pingamizi la kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles