24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

DIT na fursa za Mradi wa RAFIC

Na Hassan Daudi, Mtanzania Digital

KATIKA nchi zilizopiga hatua kiuchumi, ikitosha kuzitolea mfano Marekani na China, zimekuwapo jitihada za kuwekeza katika kuimarisha umahiri wa rasilimali watu.

Serikali nyingi zimekuwa zikitumia fedha nyingi kusomesha au kuratibu mikakati ya kuwajengea uwezo watu wake ili waweze kumudu ushindani ulioko sokoni.

Ni kwa maana hiyo basi, Benki ya Dunia (WB) kwa kushirikiana na nchi tatu za Afrika Mashariki (Tanzania, Kenya na Ethiopia) ziko kwenye utekelezaji wa mradi mkubwa wa Kuimarisha Umahiri uitwao East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP).

Aidha, sekta nyeti zilizolengwa katika utekelezaji wa mradi huo ni usafiri, nishati, uzalishaji, na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Huku Ethiopia ikiwa na vituo saba, Kenya vitano, Tanzania kwa upande wake ina vinne, kikiwamo Taasisi ya Teknolojia Dar es Saalam (DIT) kilichojikita katika TEHAMA, na Chuo cha Ufundi cha Arusha kitakachosimamia nishati.

DIT kushughulika na TEHAMA

Kwa miaka ya hivi karibuni, ukweli ni kwamba TEHAMA imekuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi, hasa kwa nchi zinazoendelea.

Unaweza kuweka kando kompyuta na kufikiri simu za mkononi zilivyogeuka nyenzo muhimu katika uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii, Taifa na duniani kwa ujumla.

Kupitia simu, watu wa kawaida wanajiingia kipato kupitia biashara wanazofanya mitandaoni, huku Serikali nyingi sasa zikivuna mapato kupitia makato ya miamala inayofanyika. TEHAMA ni fursa mpya kiuchumi.

Hebu fikiria namna utumizi wa kompyuta ulivyoleta tija kubwa katika sekta ya uzalishaji. Si tu kifaa hicho kimerahisisha kazi na kuokoa muda mwingi uliokuwa ukitumika kabla ya uvumbuzi wake, bali pia umesaidia kupunguza gharama, ambazo zingetokana na utegemezi wa idadi kubwa ya rasilimali watu.

Ni kutokana na unyeti wa sekta hiyo, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imelibeba jukumu la utekelezaji wa mradi huo kupitia Kituo cha Umahiri cha TEHAMA (RAFIC- Regional Flagship ICT Center).

DIT ni taasisi kongwe katika teknolojia hapa nchini, ambapo imekuwa ikishirikana na viwanda na mawalaka wa Serikali katika kuibua na kuziendeleza teknolojia mbalimbali, kama unavyoweza kutolea mfano uboreshaji wa mfumo wa taa za barabarani.

Serikali imekuwa ikinufaika pakubwa na wataalamu wa Taasisi hiyo kwa kuwatumia katika tafiti mbalimbali za TEHAMA, nishati, vyanzo vya maji, n.k.

RAFIC ni nini?

Akiuelezea Mradi huo, Mratibu wa RAFIC wa DIT, Dk. Joseph Matiko, anasema: “Ni mradi mkubwa wa miaka mitano ulioanza mwaka 2019, ambapo Benki ya Dunia imetoa Dola za Marekani milioni 75.

Anasema mradi wa RAFIC wa DIT unajikita katika uimarishaji wa stadi za kidigitali. “Hapa kuna stadi za msingi (basic skills), yaani kuhakikisha hata watu wa chini wanaweza kutumia kwa ufanisi vifaa vya kama simu katika shughuli zao.

“Pia, tuna ‘standard skills’, ambapo hapa unapeleka umahiri kwenye mifumo rasmi ya elimu, mfano madaktari, waalimu n.k.

“Lakini pia, kuna kundi la wabobezi. Wote wanahusika katika kuimarishiwa umahiri wao wa utumizi wa vifaa vya TEHAMA,” anasema.

Zipi faida za RAFIC?

Kama ilivyo miradi mingine ya kimkakati, RAFIC pia una faida lukuki kwa mtu mmoja mmoja, Taifa na Kikanda. Kivipi? Dk. Matiko anafafanua akisema:

“Hakuna namna ya kukwepa mikakati ya kuimarisha umahiri wa utumizi wa vifaa vya TEHAMA. Kwanza, kumekuwapo na ongezeko la vifaa vya kidigitali, mfano simu, kompyuta n.k.

“Pia, huduma nyingi kwa miaka ya sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao, achilia mbali mitandao ya kijamii. Ni kwa maana hiyo basi, kunahitajika uelewa wa utumiaji wa vifaa vya TEHAMA ili kuwapo kwa usalama.”

Kwa upande mwingine, msomi huyo anazungumzia namna Mradi huo ulivyo na tija katika dhana ya uchumi wa viwanda hapa nchini akisema umejikita katika kusaidia miradi ya kimkakati inayoanzishwa na Serikali.

“Nikigusia Kitaifa, unaweza kujiuliza, kwanini tunauhitaji Mradi huu? Jibu ni kwamba lazima tukubaliane kuwa miradi yote ya Serikali inahitaji wataalamu, watu wenye umahiri wa kuitekeleza.  Nikitolea mfano SGR au mradi wa kufua umeme.

“Huko kote kunahitaji watu waliopitia mafunzo na wenye ufanisi. Ni kama ilivyo kwa taasisi za Serikali, kwa mfano benki, ambako pia kunahitaji rasilimali-watu walioi na umahiri katika utendaji kazi wao. Kupitia RAFIC, sisi DIC tunajikita katika kuboresha umahiri wa wataalamu hao.

“Nikija Kikanda, kwa maana ya faida za nchi kwa nchi zitokanazo na RAFIC, bila shaka tunafahamu kuhusu ‘Single-Digital Market’. Sasa kama sisi tutakosa umahiri wa TEHAMA, basi tutajikuta tukiachwa nyuma na majirani zetu watakaochangamkia fursa za masoko,” anasema.

Yapi matarajio ya RAFIC?

Matarajio ya DIT endapo Mradi huo wa RAFIC utakamilika yamegawanyika katika sehemu kuu tatu. Mosi, ni uboreshaji wa miundombinu. Pili, ni ongezeko la udahili wa wanafunzi. Tatu, ni upitiaji na ongezeko la programu za masomo.

Juu ya miundombinu, Dk. Matiko anasema: “Kufikia mwishoni mwa Mradi huo mwishoni mwa mwaka 2024, matarajio ni kukamilika kwa jengo la RAFIC, ambalo litakuwa na ofisi za wakufunzi, madarasa, na bweni kwa ajili ya wanafunzi, watafiti, au wakufunzi wanaotoka nje ya nchi.

“Tumelenga kuwa na eneo la uzalishaji wa filamu na matangazo ya redio na runinga. Pia, tuwe na miundombinu ya kimtandao itakayowawezesha wanafunzi kupata maarifa.”

Akizungumzia udahili, Dkt. John Msuba, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Viwanda cha DIT, anasema kufikia mwishoni mwa mradi, kwa maana ya mwaka 2024, wanatazamia udahili wa wanafunzi uongezeke na kufikia 8,250.

“Hata hivyo, tunatupa jicho zaidi katika udahili wa wanafunzi wa kike, ambapo kwa sasa ni asilimia 15 tu. Tunataka Mradi huu utufikishe kwenye udahili wa asilimia 25,” anasema Dk. Msuba.

Akielezea hilo zaidi, Dk. Msuba anasema uchache wa wa wanafunzi wa kike wanaojiunga na kada mbalimbali DIT umechangia kuwapo kwa pengo kubwa katika uajiri, ambapo wakufunzi wengi ni wanaume.  

“Katika jitihada za awali, tumekuwa tukiwapeleka waajiriwa wetu wachache wa kike mashuleni kwa lengo la kuhamasisha watoto wa kike kufuata nyayo zao kwa kujikita kwenye masomo ya sayansi.

“Waandishi wa habari pia mna nafasi kubwa ya kumasisha wanafunzi wa kike kuja kujiunga na programu zetu hapa DIT ili kufikia lengo hili la kuongeza udahili na kupunguza pengo la kijinsia lililopo,” anasisitiza.

Utekelezaji wa RAFIC ukoje?

DIT ina njia zake za kupita katika kufikia matarajio ya Mradi wa RAFIC, moja wapo ikiwa ni kuboresha mafunzo na huduma za TEHAMA. “Hii ni kwa kutumia wakufunzi mahiri, sambamba na vifaa vya kisasa vya kufundishia.

“Tunaposema uboreshaji wa aina ya utoaji wa mafunzo, ni kwamba sasa tunasisitiza zaidi wanafunzi kushiriki kwa asilimia kubwa katika kujifunza na si kusubiri mwalimu awape kila kitu na wao kubaki kuwa wasilizaji.

“Katika nadharia hii, mwalimu anabaki kuwa msimamizi, huku mwanafunzi akiwa muhusika mkuu katika mchakato wa kujifunza,” anasema Dk. Matiko.

Vilevile, anaeleza kuwa Mradi wa RAFIC unatilia mkazo waalimu kujengewa uwezo na hii imefanyika kwa njia mbalimbali, kubwa zikiwa ni kutafutiwa nafasi viwandani ili kuimarisha umahiri wao, semina za ndani, na kupewa fursa za kusomeshwa nje ya nchi.

Huku Mradi huo ukilenga katika kuongeza udahili wa wanafunzi katika programu mbalimbali, pia lipo suala la kuongeza programu ili wanaotoka nje wavutiwe kuja nchini.

Juu ya kupitia mitaala ya programu, Dk. Matiko anasema: “Lazima tujiridhishe juu ya uhai wa kile tunachofundisha, kuona kama kinakubaliana na mazingira halisi. Hii itatusaidia kuandaa vijana wanaoendana na mahitaji ya soko la sasa. Ni kwa maana hiyo basi, lazima mitaala wanayotumia iwe inapitiwa na kuona kama bado inakidhi mahitaji.”

Dk. Matiko anasisitiza kuwa Mradi wa RAFIC pia umejikita katika kushahuri na kutatua changamoto za usalama wa kimtandao na uboreshaji wa tafiti na gunduzi mbalimbali.

Ni kama anavyosema Dkt. Msuba, alipoeleza utayari wa DIT kushirikiana na taasisi zingine. “DIT tuko tayari kabisa kuzisaidia taasisi zingine katika miradi yake kwa kuzipa wataalamu, kama ambavyo tumekuwa tukitumia rasilimali-watu tulizonazo kutatua changamoto zetu hapa chuoni.”

Dk. Matiko anaongeza kwa kusema jicho la Mradi wa RAFIC pia liko pia kwenye ujenzi wa jengo litakalotumika kwa mafunzo ya utengenezaji wa masanamu yanayotumika katika uzalishaji mali na kutoa huduma (Robotic and Artificial Intelligence Lab).

“Huko ndiko dunia inakotaka tufike katika karne hii ya 21. Unaweza kusikia kuhusu magari yasiyo na dereva. Sasa vipi utakaponunua, halafu limeharibika? Ina maana utarudisha Ulaya. Tunapaswa kujiandaa kwa kuwapika wataalamu wetu ili waweze kushughulika na changamoto hiyo,” anasema Dkt. Matiko.

Mradi umefikia kiwango gani?

Kwa miaka miwili ya utekelezaji wa mradi, yapo mengi DIT inajivunia. Je, unajiuliza ni yapi hayo?  Anayefafanua ni Daudi Mboma, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa RAFIC katika Taasisi ya DIT.

“Nianze kwa kusema udahili wa wanafunzi umeongezeka kwa kasi ya kuridhisha. Nikitolea mfano, mwanzoni mwa Mradi, tulikuwa na udahili wa wanafunzi wa TEHAMA 434 lakini mwaka huu tuna 2494, huku wa kike wakiwa ni 363,” anasema Mboma.

Mbali ya mafanikio hayo, anasema kwa kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji, wameweza kuwafutilia wahitimu wetu na kubaini kuwa wengi wao (60%) wameajiriwa mara tu walipomaliza masomo.

“Vilevile, katika ufuatiliaji huo, wengi (74%) walikiri kufanya kazi zinazohusiana na kile walichosoma chuoni hapo.

“Tumefanikiwa pia kuanzisha Tume ya Ushahuri wa Viwanda, ambayo inaundwa na wataalamu tisa, baadhi yao wakiwa ni watalaamu wetu hapa DIT. Wataalamu wengine wanatoka katika viwanda ili kuongezea uzoefu wa maeneo ya kazi.

“Tumeshiriki miradi mbalimbali ya kimkakati ya Kikanda kwa kushirikiana na wadau wetu wa nje, sambamba na kupitia mitaala ya programu nane na zimeshaanza kutumika,” anaongeza Mboma.

Anayataja mafanikio mengine ya DIT kupitia Mradi huo ni kupeleka waalimu nje ya nchi, ambapo wawili wamesharejea nchini wakitokea Uingereza walikokuwa wakisomea Shahada ya Uzamili (Masters) ya Usalama wa Mitandaoni (Cyber Security).

“Ukiacha hao waliokwenda na sasa wanaendelea na majukumu ya kunoa vijana hapa chuoni, wapo wengine wanaotarajiwa kwenda hapo baadaye. Hao ni mbali ya waliopatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo hapa hapa nchini kupitia semina na kuwapeleka katika viwanda mbalimbali,” anasema.

Je, kuna hatari ya Mradi kuchelewa kukamilika?

Ikiwa ni takribani miaka mitatu imebaki kufikia mwaka 2024, Taasisi ya DIT haioni kama itachelewa kukamilisha Mradi wa RAFIC.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Taasisi hiyo, Profesa Preksedia Ndomba, hatua za utekelezaji zinakwenda vizuri, hata ukilinganisha na nchi zingine zilizo kwenye mradi huo.

“Unajua unaweza kuona tumetumia miaka miwili lakini si kweli kwamba inafika. Tulichelewa kiasi na hiyo ilitokana na janga la Corona lililokuwa limeshamiri mwaka 2019.

“Hivyo, sisi ni tulianza utekelezaji mwaka 2020. Ni kweli kwa Tanzania haikuwa tatizo kubwa lakini tulihitaji nchi zingine ziwe huru ili kurahisha utendaji kazi kwa kuwa baadhi ya vifaa vilipaswa kuagizwa nje,” amesema.

Mwisho, Prof. Ndomba anaongeza kuwa wawakilishi wa Benki ya Dunia walitembelea na kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles