Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa klabu ya JKT Ruvu, umesema unakabiliwa na deni kubwa la kuhakikisha kikosi cha timu hiyo kinaimarishwa katika usajili wa dirisha dogo, ili kiweze kuanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kikiwa na mabadiliko makubwa.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Constatine Masanja, aliliambia MTANZANIA jana kuwa, ripoti ya kocha Malale Hamsini ndiyo itakayowapa mwongozo katika kufanya marekebisho ambayo wanaamini yataisadia timu yao kwenye mzunguko wa pili.
“Kocha tayari amewasilisha ripoti yake na tunatarajia kukutana leo au kesho kuijadili ili tuweze kuanza mchakato wa usajili kwa kuyafanyia kazi mapendekezo yake,” alisema.
Alisema safu ya ushambuliaji itapewa kipaumbele katika maboresho yatakayofanywa kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika duru la kwanza, huku akisisitiza usajili utafanywa kwa umakini mkubwa.
Masanja alisema hawatabweteka katika mzunguko wa pili badala yake watapambana zaidi katika hatua hiyo ili kupata matokeo yanayoridhisha ambayo yatawawezesha kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi.