28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Murray atwaa ubingwa wa dunia wa ATP

LONDON, ENGLAND


andy-murray

BINGWA namba moja kwa ubora wa mchezo wa tenisi duniani, Mwingereza Andy Murray, amefanikiwa kunyakua tuzo ya kwanza ya fainali za dunia za ATP 2016, baada ya kumshinda mpinzani wake, Novak Djokovic.

Murray amekuwa na kiwango cha hali ya juu tangu mwanzo wa msimu huu, huku kwenye fainali hizo za ATP ameweza kumchapa mpinzani wake kwa seti 6-3 6-4, mchezo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa O2 Arena mjini London.

Murray amefanya mapinduzi ya kuwa mchezaji bora duniani mapema mwezi huu, baada ya kumpindua mpinzani huyo ambaye alikuwa anashikilia nafasi ya kwanza kwa ubora.

Murray anaamini ubingwa huo ambao ameupata jana ni wazi kuwa yeye ni bora duniani kwa kuwa ameweza kumgaragaza nyota ambaye alikuwa anashika nafasi ya kwanza kwa ubora duniani.

“Kwanza kitu ambacho kila siku kinanifanya nijisikie kuwa mtu mwenye furaha ni kuwa bingwa namba moja kwa ubora duniani katika mchezo huu, hiyo ni nafasi ambayo nilikuwa ninaitafuta mara kwa mara katika maisha yangu ya mchezo huo.

“Lakini furaha nyingine ambayo ninayo kwa sasa ni ushindi nilioupata dhidi ya mpinzani wangu Djokovic, siku zote amekuwa akifanya vizuri hivyo ushindi wangu ni furaha kubwa kwa kuwa ni hatua nyingine na nimeweza kumshinda yule ambaye alikuwa anatamba kwa ubora duniani,” alisema Murray.

Murray mwenye umri wa miaka 29, amedai kuwa alikuwa na kipindi kizuri msimu huu kutokana na maandalizi ambayo aliyafanya kwa kipindi kirefu.

“Nimeweza kufika hapa kutokana na maandalizi ambayo niliyafanya kwa kipindi kirefu, haikuwa kazi nyepesi kuweza kufika hapa kwa kuwa kila siku niliweza kukutana na ushindani wa hali ya juu.

“Katika fainali hizi, niliujua ubora wa Djokovic, hivyo nilitumia nguvu nyingi sana kwa ajili ya kuweza kupambana na nyota huyo, hivyo nashukuru nimeweza kufanikisha kile ambacho nilikuwa nakikusudia,” aliongeza.

Kwa upande wa Djokovic, naye amedai kuwa alikutana na ushindani mkubwa kutoka kwa mpinzani wake Murray na nyota huyo namba moja kwa ubora duniani amestahili kutwaa taji hilo.

“Murray alikuwa katika ubora wa hali ya juu na ndio maana amefanikiwa kuchukua taji hilo la ATP, ninaamini alikuwa na maandalizi mazuri tangu mwanzo wa msimu huu na ndio maana aliweza kufanya vizuri hata katika michuano mingine iliyopita,” alisema Djokovic.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles