AMSTERDAM, NETHERLANDS
BEKI wa Ajax, Matthijs de Ligt, amethibitisha kuwa hakuna klabu ya ndoto yake iliyojitokeza hadi sasa licha ya kutakiwa na klabu nyingi barani Ulaya ikiwamo Barcelona na Man United.
De Ligt (19), amekuwa akigombewa na klabu kubwa barani Ulaya zikihitaji kumsajili kwa ajili ya msimu ujao, lakini beki huyo anataka kuendelea kucheza Ajax msimu ujao.
Mbali na klabu hizo, pia Juventus na Liverpool zimedaiwa kuifukuzia saini ya beki huyo ambaye alifanikiwa kuiongoza Ajax kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Licha ya De Ligt kutokuwa na haraka ya kufanya uamuzi kwa sasa, mkataba wake unamalizika mwaka 2021.
De Ligt aliueleza mtandao wa NOS: “Sijafanya uamuzi wowote kwa sasa.
“Mambo mengi yanaandikwa na kusemwa kuhusu mimi. Lakini hayajawahi kunifanya nichanganyikiwe.
“Frenkie de Jong (ambaye amejiunga Barcelona) alishafanya uamuzi wake lakini mimi bado, huo ndio ukweli.
“Unatakiwa kuangalia kile kilicho bora kwako kisha ndio ufanye uamuzi, nafahamu klabu nyingi zinanihitaji, ni jambo zuri.”
De Ligt aliongeza: “Sina ndoto ya klabu nyingine tofauti na Ajax. Kila siku imekuwa ndoto yangu na kupata mafanikio nikiwa hapa.
“Naangalia klabu bora kwa kazi yangu ambayo itakuwa sehemu sahihi kuendeleza kipaji changu. Lakini bado nina mkataba na Ajax, hivyo msimu ujao nitakuwa hapa.”