Na Clara Matimo, Mtanzania Digital
Leo ni Agosti 23, 2022, Taifa la Tanzania liko katika zoezi la sensa ya watu na makazi ambapo Mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Thomas Apson, ametoa rai kwa wananchi wilayani humo kukaa majumbani mwao ili wasubiri kuhesabiwa.
Apson ametoa rai hiyo Agosti 22, 2022 zikiwa zimebaki saa chache zoezi la sensa kufanyika nchini wakati akizungumza na Mtanzania Digital kuhusu kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki zoezi la sensa linalofanyika kuanzia leo ngosti 30, mwaka huu.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan aliitangaza Agosti 23, 2022 kuwa siku ya mapumziko kutokana na umuhimu wa zoezi la sensa kwa kuwa linaenda kutengeneza dira nzuri kwa maendeleo ya mtanzania katika kipindi cha miaka 10 ijayo pamoja na kuisaidia serikali kutambua mahitaji muhimu ya wananchi wake na changamoto walizonazo ili ipange jinsi ya kuzitatua.
“Kesho Agosti 23, 2022 (leo) ni siku muhimu sana tunajenga msingi mkubwa sana wa kumuendeleza mtanzania kwa hiyo kila mtu awe tayari kuhesabiwa asiwe mkaidi, asiseme amechoka maswali maana maswali hayo utaulizwa kwa dakika chache tu na maswali hayo yataenda kuwasaidia zaidi mbeleni katika kufaidika kwa kupata huduma nzuri na bora za kijamii ambazo kila mtanzania anapenda kuzipata ikiwemo maji, umeme, shule za kutosa na zahanati.
“Ni siku muhimu sana kwa watanzania wote wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Siha wote kwa pamoja tuhakikishe tunashiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ili baadaye tusije kuanza kuilaumu serikali mbona haitutatulii changamoto hii tuliyonayo maana takwimu zitakazo kusanywa zitaisaidia serikali kuwapatia wananchi wake mahitaji wanayoyahitaji kwa ufanisi zaidi kwani itajua watu inaowahudumia ni wa aina gani, wako maeneo gani na wanauhitaji wa kitu gani,”alisema Mkuu huyo wa wilaya na kuongeza
“Yote haya yatafanyika kwa usahihi na uhakika zaidi au kwa kiingreza with precision and quality endapo watanzania wenzangu sehemu mbalimbali ikiwemo wananchi wa Wilaya ya Siha watatoa ushirikiano kwa kuwa tayari kuhesabika au kusensabika siku ya kesho(leo) na kuendelea lakini uzuri ni kwamba Siha tunasema kwa kauli moja tupo tayari kusensabika,”amesema Apson.
Apson ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya sensa Wilaya ya Siha amesema zoezi la sensa linafaida kwa Watanzania wote wakiwemo viongozi na wanaoongozwa ambapo alibainisha kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ni rais ambaye amefanya mambo makubwa kwa muda wa mwaka mmoja akiwa madarakani ambayo kiongozi mwingine katika nchi nyingine ingemchukua miaka mitatu hadi minne kuyafanya.
Aliendelea kusema kwamba ni rais ambaye ameonekana kuwa na kasi ya kuwaletea wananchi wake maendeleo anachohitaji ni takwimu sahihi za watu anaowahudumia ili aweze kupanga jinsi ya kuwapa huduma muhimu hivyo kila mwananchi asikubali kukosa kuhesabiwa.
“Kule mbuga za wanyama Ngorongoro ni porini lakini leo hii kuna foleni ya magari haijawahi kutokea hii ni kutokana na aina ya rais tuliye naye, tuna rais mwenye kasi tunayoihitaji, tuna rais anaye jali wananchi wake, tuna rais mnyenyekevu yeye pamoja na serikali yake, ametuambukiza haiba yake na sisi wasaidizi wake tunaomsaidia tuko tayari muda wote kuwahudumia wananchi sasa ili tufanye vizuri zaidi kila mmoja wetu awe tayari kusensabika,”amesema Apson.