29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango: Viongozi wa Dini saidieni malezi ya Watoto

*Ahimiza wazazi kuacha ukimya na kuzungumza na watoto wao

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango amewahimiza Viongozi wa Dini pamoja na wale wa kimila kushirikiana na Serikali katika kulea watoto kimaadili ili kuepusha vitendo viovu na visivyopendeza katika jamii.

Sehemu ya washiriki wa mkutano huo.

Aidha, amewaasa wazazi wote katika nchi za Afrika kujitahidi kufuatilia maendeleo ya Watoto shuleni pamoja na kuzungumza nao ili kuweza kutatua changamoto wanazopitia na kuwasaidia kutumia maarifa, ujuzi na vipaji walivyonavyo kwa maendeleo ya bara la Afrika.

Dk. Mpango ametoa rai hiyo leo Jumatatu Agosti 22, 2022 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Mkutano wa 13 wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya za Skauti wa Kike (Girl Guides) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watoto wa Tanzania Girl Guides.

Amesema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kuhimiza malezi bora ndani ya jamii sababu wanasikilizwa na watu wengi hivyo ni muhimu kutilia mkazo jamo hilo ili kujenga jamii salama na yenye maadili.

“Niwaombe viongozi wa dini zetu nchini kushiriki kikamilifu katika kusaidia malezi ya watoto wetu, kwani iwapo wataandaliwa vyema kwenye misingi bora ya dini watakuwa ni tegemeo bora la taifa la kesho na Bara letu la Afrika kwa ujumla, hivyo tukishindwa kufanya hivyo leo basi tutalia kesho.

“Pia niwaombe wazazi na walezi ndani ya jamii zetu tuache ukimya, tuzungumze na watoto wetu tuwafundishe kuhusu maadili kwani kuporomoka kwake ndiyo imekuwa sababu ya vitendo viovu.

“Katika hlii niwaombe wazazi wetu kuyashika yale yanayofundishwa na Tanzani Girl Guide kwa watoto wetu, jukumu la malezi ni shirikishi hivyo niwasihi wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kushirikiana pamoja katika malezi ya watoto. Barani Afrika watoto wengi wanafanyiwa ukatili sababu wazazi hatuongei na watoto wetu,” amesema Dk. Mpango.

Katika hatua nyingine Dk. Mpango ameipongeza Girl Guide kwa kusema kuwa imekuwa ni moja ya nyezo bora katika kutayarisha viongozi bora wanawake barani Afrika.

“Girl Guide imekuwa chachu ya kutengeneza viongozi bora wanawake na wenye mchango kwenye mataifa mengi ya bara letu, hatuna budi kustawi pamoja ili tulete maendeleo kwenye bara letu na ili kulifanikisha hilo lazima tutembee pamoja na Girl Guide.

“Kuporomoka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya katika nchi za Afrika ambalo linachangia kurudisha nyuma jitihada za maendeleo na kuondoa umasikini, Jumuiya hizi katika mataifa zinapaswa kushirikiana na serikali pamoja na wazazi husasan wakati huu wa utandawazi ili kuepusha vitendo vya mmomonyoko wa maadili,” amesema Dk. Mpango.

Dk. Mpango pia amehimiza wadau wa maendeleo kuiwezesha Tanzania Girl Guides ili iweze kufika katika kila pembe ya nchi hususan maeneo ya vijijini.

“Pia nitoe rai kwenye kufika katika maeneo ya vijijini pia kuhimiza watoto wakike wakiwamo wakina mama na wasichana kujiunga na Tanzania Girl Guides kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kujitambua na kujithamini.

“Niwasihi wadau wa maendeleo kukiwezesha chama hiki ili kiweze kufikia wanawake wengi zaidi nchini kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa na taifa imara na jamii isiyo na ukatili wala utapia mlo,” amesema Dk. Mpango.

Kuhusu chama hicho kushirikishwa kushirikiashwa kwenye shughuli za kiserikali, Dk. Mpango amemuagiza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima kwa kushirikiana na Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda kuhakikisha kuwa wanafanyia kazi suala hilo.

Aidha, juu ya Tanzania Girl Guides kutengewa ruzuku serikali Dk. Mpango amesema kuwa watapitia sera kuona zinavyosema.

Awali, Kamishna wa Tanzania Girl Guides, Mary Richard amesema kuwa changamoto zinazowakabili ni ukosefu wa ruzuku na hivyo kuomba uwezeshwaji kutoka serikalini.

“Tunatamani kuona vijana wetu wakishirikishwa kwenye shughuli za kiserikali ili iweze kuwajengea nguvu ya kuwa imara na jasiri.

“Jambo jingine ni changamoto ya urasimishaji wa mkataba kutokana na mazingira ya awali ya kuingiwa mkataba, pia kipaumbele chetu kingine ni juu ya upatikanaji wa sheria inayotuhusu sisi,” amesema Mary.

Ameongeza kuwa Tanzania Girl Guides imekuwa ikitoa elimu ya kupunguza madhara yatokanayo na ulevi, pombe, elimu ya hedhi salama, lishe bora, hedhi salama, ndoa na mimba za utotoni na ujasiriamali.

“Tunaendelea kuwajengea uwezo wa kujiamini pamoja na kutengeneza viongozi wenye maadili mema,” amesema Mary.

Upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima alisema kuwa kwasasa tayari wamekamilisha programu ya malezi ya Desemba 2021 yenye lengo la kumkuza mtoto kwa utimamu wake katika ulinzi na afya bora.

“Pamoja na hilo tuna Mkakati wa Mei 2021 ambao unalenga kupunguza mambukizi ya Virusi Vya Ukimwi, Ndoa za Utotoni, mimba za utotoni na Ukeketaji.

“Pia tuko kwenye hatua za mwisho za mapitio ya sera ya mtoto ya mwaka 2000 ili kuona namna gani itaweza kuendana na mazingira ya sasa lakini pia Katibu Mkuu wa Wizara atapeleka nakale kwenye chama cha Tanzania Girl Guides ili kiweze kupitia na kutoa mapendekezo yake,” amesema Dk. Gwajima.

Mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kitaifa wa Maliwamu Julias Nyerere ukiwa na kaulimbiu ya “Tusitawi pamoja, rudisha mstakabali wa Bara la Afrika kwa kutumia marifa, ujuzi na vipaji vya Wanawake Vijana” ukihusisha nchi wananchama 33 za Afrika unatarajiwa kuhitimishwa Agosti 26, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles