31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

DC Makilagi: Watakaokwamisha zoezi la Sensa ni wahalifu kama wahalifu wengine

*Asema watakaobainika Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria

Na Clara Matimo, Mwanza

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi, amewaonya watu watakaokwamisha zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajia kufanyika Agosti 23, 2022 kwani kufanya hivyo ni uhalifu kama uhalifu mwingine hivyo serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habri wa Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania(OJADACT), Edwin Soko akizungumza kwenye semina ya mafunzo ya kuandika habari mwendelezo za sensa kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya kanda ya ziwa (hawapo pichani).

Amesema Sensa ipo kwa mujibu wa sheria hapa nchini tangu mwaka 1967, mtu yeyote atakayebainika kukwamisha zoezi hilo atakuwa anakiuka sheria hivyo sheria itachukua mkondo dhidi yake.

Makilagi ametoa onyo hilo Agosti 20, 2022 wakati akifungua semina ya mafunzo ya kuandika habari mwendelezo za sensa kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya kanda ya ziwa iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habri wa Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania(OJADACT).

Makilagi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya sensa Wilaya ya Nyamagana amesema sensa ni muhimu kwa maendeleo ya taifa hata Mwenyezi Mungu anatambua umuhimu wa sensa ndiyo maana imeandikwa katika vitabu vitakatifu vya dini za kiislamu na kikristo ambavyo ni Biblia na Quran.

“Ukisoma Biblia Takatifu Luka 2:1-7 utaona inavyoeleza kuhusu sensa, quran Tukufu nayo tunaona Mtume Mohamed(S.W.A) alisafiri hadi akaingia Maka alipofika huko kabla hajaendelea na safari yake ya kuelekea madina alikutana na umati wa watu Mwenyezi Mungu akamwambia waulize wako wangapi hivyo walihesabiwa kwa hiyo vitabu vyote vinaonyesha umuhimu wa zoezi la sensa.

“Ombi langu kwenu waandishi wa habari isaidieni serikali  kuielimisha jamii asitokee mtu yeyote akapotosha suala la sensa maana lipo hapa nchini kwa mujibu wa sheria, ukweli usiopingika asilimia kubwa ya jamii imepata elimu kuhusu umuhimu wa sensa kupitia nyie waandishi wa habari, hata tafiti zinaonyesha  sensa zilizotangulia waandishi wa habari mlikuwa ni mabalozi wazuri,”amesema Makilagi.

Amefafanua kwamba matokeo ya sensa ya watu na makazi yataiwezesha serikali kupata picha kamili juu ya watu waliomo nchini hivyo yatakuwa ni msingi katika kupanga  mipango ya maendeleo  kiuchumi na kijamii ikiwemo elimu na afya.

Amesema maandalizi yote ya sensa yamekemilika kwa asilimia 100 wilayani humo na watu wote watakaolala ndani ya mipaka hiyo usiku wa kuamkia siku ya sensa watahesabiwa wakiwemo watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, wasafiri na wenye matatizo ya akili kwani wameweka mazingira rafiki ya kuwafikia.

“Ninachoomba ni wananchi wote ambao ni  wakuu wa kaya kutoa ushirikiano kwa makarani wetu siku hiyo kwani tutaanza zoezi la sensa saa 6:01 usiku wa kuamkia siku ya sensa na hivi tunavyozungumza tayari makarani wetu ambao watakwenda kulala mkoani Kagera wameishateuliwa watakuja na meli ikifika muda huo wataanza kuhesabu watu hadi meli inatia nanga hapa Mwanza watakuwa wameishamaliza zoezi hilo ndani ya meli,”ameeleza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa OJADACT, Edwin Soko, amesema lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari waweze kuandika habari za mwendelezo kuhusu sensa zitakazukuwa na tija kwa jamii na taifa kwa ujumla huku akibainisha kwamba imefadhiliwa na wafadhili mbalimbali akiwemo  Cecy Toto Gift shop na Taasisi ya Desk and Chair Foundation.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles