22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

DC Nyamagana atishwa na mimba za utotoni

Baraka Konisaga
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga

Na Charles Mseti, Mwanza

MKUU wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, amesema nchi inahitaji mpango mkakati ili kuwawezesha vijana kuondokana na ongezeko la mimba za utotoni.

Konisaga alisema hayo juzi alipokuwa akifungua mkutano juu ya idadi ya watu duniani uliofanyika jijini hapa.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kumekuwapo ongezeko kubwa la vijana wa umri chini ya miaka 18 kuingia katika ndoa hali inayosababisha uchumi kushuka.

Konisaga alisema Serikali inapaswa kutilia mkazo na kusimamia maeneo muhimu ikiwamo sekta ya elimu, afya ya uzazi wa mpango itakayowezesha vijana wengi kukabiliana na changamoto za maendeleo.

“Ukiangalia takwimu za sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2012 katika Mkoa wa Mwanza, inaonyesha idadi ya vijana walio kati ya miaka 10 hadi 24 ni 906,171 sawa na asilimia 32.6 ya wakazi wote wa mkoani hapa, hivyo basi kuwekeza kwa vijana ni suala lenye umuhimu mkubwa katika maendeleo ya sasa.

“Tunajua kabisa Serikali yetu inatilia mkazo mkubwa katika kuwekeza kwa vijana wa kike na wa kiume ili kuweza kushiriki kikamilifu na kuchangia katika shughuli za kujiendeleza kielimu na uzalishaji mali itakayoweza kuchangia katika pato la taifa,” alisema.

Naye Mchumi Mkuu wa Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, Edwin Ninde, alisema kumekuwapo ongezeko kubwa la vijana walio chini ya umri wa miaka 18 nchini wanaojifungua kabla ya wakati kitendo ambacho ni hatari katika uchumi wa taifa.

Ninde alisema juhudi za ziada zinahitajika ikiwa ni pamoja na Serikali kupinga kwa nguvu ndoa za utotoni ambazo zinaonyesha kwa kiasi kikubwa kuchangia kudorora kwa uchumi wa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles