24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

DC Nguvila: Jiungeni na uvuvi endelevu kukomesha uvuvi haramu

Renatha Kipaka, Muleba

Kutokana na mwendelezo wa zoezi la kutokomeza uvuvi haramu, kikosi kazi kilichoundwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera kimeendelea na doria za mara kwa mara na kufanikiwa kukamata watu wanaojihusisha na uvuvi haramu wakiwa na zana haramu

Zana zinazotumika kuvua Samaki kiharamu, ni kokoro na timba zenye thamani ya Sh milioni 16 na samaki waliovuliwa kwa kutumia zana haramu hizo ni tani sita zenye thamani ya Sh milioni 10.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Usalama ya Wilaya, Toba Nguvila ameendelea kuwasihi wavuvi haramu kuacha mara moja biashara hiyo kwani itawapelekea kubaya.

“Uvuvi haramu unadhoofisha sana uvuvi endelevu kwenye wilaya ya Muleba na mkoa mzima wa Kagera. Wavuvi hawa mtandao wao ni mkubwa, Waliokamatwa ni mabingwa wa kuingiza zana haramu kupitia mipaka mbalimbali kutoka nchi za nje ili kuwawezesha wavuvi haramu waliopo ndani ya nchi,” amesema Toba.

Aidha, ametoa rai kwa wavuvi wanaojishughulisha na biashara hii haramu kuwa ni vema wakajiunga na uvuvi endelevu, uvuvi wa kihalali kwa kutumia nyavu zilizothibitishwa na Wizara na ambazo hazileti madhara katika mazalia ya samaki.

Kwani iko hatari katika uvuvi haramu itakayopelekea kupoteza mazao ya samaki kwenye maziwa, kupoteza ajira kwa waliojiajiri kupitia uvuvi endelevu na kupoteza mapato mengi ambayo Serikali inayapata kupitia Uvuvi endelevu.

Pia amewaonya wavuvi kuacha kuvua samaki walio chini ya viwango kwani kikosi kazi kipo kazini na kinaendelea na zoezi la kuwabaini na kuwakamata wote wanaojihusisha na uvuvi haramu, hivyo kwa wanaondelea watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya kisheria.

Ameendelea kueleza kuwa uongozi upo imara na kadri siku zinavyokwenda ndivyo wanavyoongeza nguvu katika kukabiliana na wavuvi haramu kutokana na mtandao wao kuwa mkubwa.

Aidha amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri na kwamba zitaendelea kuwa za siri ili kukabiliana kutokomeza uvuvi haramu katika visiwa 39 vilivyopo wilaya ya Muleba ndani ya Ziwa Viktoria na ziwa Burigi.

Pia, Nguvila ameeleza kuwa wapo maafisa uvuvi wanaoshirikiana na wavuvi haramu kuvua samaki kiharamu na kuwasafirisha au kuwauza kiharamu hivyo amewaonya Maafisa uvuvi hao wasio waadirifu na waaminifu wanaoshirikiana na wavuvi haramu kuendeleza uvuvi huu kuwa watachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwani uchunguzi unaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles