32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

DC Mpogolo: Tumedhamiria kutatua changamoto zote za mama lishe

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema wamedhamiria kutatua changamoto za mama ili kuhakikisha wanafanya shughuli zao katika mazingira mazuri na kukuza uchumi wao.

Ameyasema hayo Machi 22,2024 wakati wa mafunzo ya mama lishe kutoka masoko ya Kisutu, Mchikichini, Buguruni, Feri, Ilala, Machinga Complex na Kigogo Sambusa.

Amesema zaidi ya Sh bilioni 6.5 zimehifadhiwa benki ambapo wanasubiri Serikali itangaze utaratibu mwingine waanze kukopesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kuwataka mama lishe kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiunga kwenye vikundi na kuvisajili.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akizungumza wakati wa mafunzo ya mama lishe kutoka katika masoko mbalimbali yaliyopo wilayani humo.

Mkuu huyo wa wilaya pia amewataka mama lishe katika Soko la Buguruni kuendelea kufanya shughuli zao wakati wakiendelea na majadiliano na Wakala wa Barabara (Tanroad) wanaotaka kuwahamisha wafanyabiashara hao.

Mmoja wa mama lishe kutoka Soko la Buguruni, Fatuma Mohammed, amesema wanatakiwa kuhama kupisha upanuzi wa barabara na kumuomba mkuu huyo wa Ilala kuwasaidia waweze kuendelea kufanya shughuli zao.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akimkabidhi mtungi wa gesi Mama lishe, Asha Mageta, wakati wa mafunzo ya mama lishe kutoka katika masoko mbalimbali yaliyopo wilayani humo. Wapili Kulia ni Meneja wa NMB Ilala, Christina Lifiga.

Changamoto nyingine zilizowasilishwa na mama lishe hao ni ukosefu wa mitaji, miundombinu mibovu ya majitaka, uhaba wa maji katika Soko la Feri na kuomba mamlaka zinazohusika kuboresha ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira salama.

Mpogolo pia amewashauri mama lishe kuungana na kuanzisha umoja wao ili iwe rahisi kushughulikia changamoto zao kama ilivyo kwa makundi mengine ya bodaboda na wamachinga.

“Kama tunao umoja wa bodaboda, bajaji tunakosaje kuwa na umoja wa mama lishe, kwenye umoja wenu ndipo mtapata mtu atakayesadia kuwatetea,” amesema.

Ofisa Lishe kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Neema Mwakasege, amesema mpaka sasa wamewafikia mama lishe 1,500 kutoka kata zote 36 za halmashauri hiyo na kuwapatia mafunzo.

“Tunatoa elimu kwa kundi hili kuhusu uandaaji wa vyakula kwa kuzingatia makundi sita muhimu ya chakula ili walaji waweze kupata mlo kamili. Tunafanya hivi ili afya za Watanzania ziendelee kuwa salama kwa sababu watu wengi wa tabaka la chini wanapata huduma ya chakula kwa mama lishe,” amesema Mwakasege.

Meneja wa NMB Ilala, Christina Lifiga, amewataka mama lishe kuchangamkia fursa mbalimbali za mikopo inayotolewa na benki hiyo ukiwemo mkopo wa ‘Jasiri’ maalumu kwa wanawake wafanyabiashara ambao amesema una riba ndogo.

Katika mafunzo hayo pia mama lishe hao walipewa elimu ya matumizi ya nishati mbadala ili kuachana na kuni na mkaa ambapo waliofanya vizuri kwenye maeneo yao walizawadiwa mitungi ya gesi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles