23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

DC Maswa azindua mfumo wa anuani za makazi na Postikodi

Na Samwel Mwanga,Maswa

Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge amezindua rasmi mfumo wa Anuani za Makazi katika Wilaya hiyo kwa kuweka vibao vya anwani katika barabara na nyumba zilizopo mtaa wa  Biafra A barabara ya Kadoto katika Kata ya Shanwa.

Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 15, 2022 ambapo DC Kaminyoge amewatangazia wananchi hao kuwa zoezi la anwani kwa Wilaya hiyo limeanza rasmi hivyo wananchi watoe ushirikiano mkubwa kwa wakusanya taarifa watakaofika kwenye maeneo yao.

Amesema zoezi hilo linafanyika ikiwa ni maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kwani lina manufaa makubwa.

“Zoezi hili  linahusisha wananchi kwa maana ya ushiriki na viongozi kwa maana ya usimamizi hivyo kila mmoja atimize wajibu wake na kikubwa hawa vijana watakaofanya zoezi hili ni vizuri wakapatiwa ushirikiano mkubwa,” amesema.

Kaminyonge ameendelea kueleza kuwa ni vizuri zoezi hilo lifanyike kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu na limalizike kwa muda uliopangwa na hata ikipidi limalike kabla ya muda uliopangwa ili waweze kupata muda wa kufanya uhakiki wa mambo mengine ambayo yatakuwa na dosari kidogo.

“Nasisitiza zoezi hili ni lazima liishe kwa wakati, ufanisi na nitapenda kwa wilaya ya Maswa tumalize kabla ya muda uliowekwa ila kama kuna kufanya usahihi wa baadhi ya taarifa tuzifanyie,” amesema Kaminyonge.

Aidha, amesema ushiriki wa mwananchi ni wa kutoa taarifa zinazotakiwa kwenye zoezi ikiwemo jina kamili la mmiliki wa nyumba au kiwanja, kitambulisho cha NIDA au namba ya NIDA kwa wale wenye navyo, namba ya kiwanja kwa vile vilivyopimwa na namba za simu.

“Kila mwananchi anaemiliki nyumba au kiwanja aache taarifa zake kwa mtu anaebaki nyumbani pindi atakapo kuwa hayupo na wapangaji wote pia wanapaswa kuwa na taarifa sahihi za wenye nyumba wao ili kurahisisha zoezi kwa wakusanya taarifa,” amesema Kaminyonge.

Kaminyoge ametumia fursa hiyo pia kueleza moja ya faida ya anwani hizo kuwa zitasaidia  kurahisisha mawasiliano, kuwezesha biashara mtandao, kuimarisha ulinzi na usalama na kuwezesha shughuli mbalimbali za kitaifa ikiwemo zoezi la sensa litakalofanyika Agosti, mwaka huu.

Awali, Afisa Ardhi wa wilaya ya Maswa, Vivian Christian amesema kuwa ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi halmashauri ya wilaya hiyo imetoa elimu kwa Wajumbe wote  wa Kamati za Maendeleo ya Kata katika Kata 36 zilizoko wilayani humo sambamba na kutangaza nafasi 630 kwa vijana watakaosaidia kukusanya taarifa za anuani za makazi na wameshafanyiwa usaili.

Amesema pamoja na utekelezaji huo pia zoezi hilo lina changamoto ikiwemo upungufu wa fedha ambapo wilaya hiyo ilipanga kutumia Sh bilioni 2.11 lakini fedha waliyopatiwa ni Sh milioni 151.60.
“Pamoja na upungufu wa  fedha ambazo tuliomba na kiasi kilichotengwa sisi kama halmashauri tutaongeza fedha hizo kupitia mapato yetu ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za anuani za makazi na Postikodi,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles