Na Samwel Mwanga, Maswa
Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge amewataka wananchi wa wilayani humo kutunza na kulinda vyanzo vya maji.
Akizungumza Septrmba 17, 2022 katika kijiji cha Zebeya kwenye uzinduzi wa ujenzi wa Mabwawa ya Ilambambasa na Zebeya wilayani humo amesema utunzaji wa vyanzo vya maji ni suala mtambuka ambalo linahusisha wadau mbalimbali wakiwamo wananchi.
Amesema kuwa wadau wakubwa na muhimu katika utunzaji wa vyanzo vya maji ni watumiaji maji na wananchi waishio katika maeneo jirani na vyanzo hivyo ni muhimu wakavilinda kwa uangalifu bila kuviharibu.
“Wadau wakubwa na ambao ni muhimu katika utunzaji wa vyanzo vya maji ni watumiaji maji na wananchi wanaoishi katika maeneo jirani vilipo vyanzo vya maji hivyo ni muhimu kuelimishwa kuhusu kutumia maji kwa busara,uangalifu na kwa tija bila kuharibu chanzo,” amesema Kaminyonge.
Aidha, Kaminyonge amesema suala la kuhifadhi vyanzo vya maji limekuwa likitiliwa mkazo na Serikali hada awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema viongozi wote katika ngazi zote wilayani humo kuwa wana wajibu wa kulishughulikia kwa mtazamo chanya suala la utunzaji wa vyanzo vya maji katika maeneo yao kama wanavyoshughulikia masuala mengine.
Aidha, amewaomba wananchi na viongozi katika vijiji hivyo ambapo yanajengwa mabwawa hayo kutoa ushirikiano wakati wote wa ujenzi wa mabwawa hadi hapo utakapokamilika na kuanza kuwahudumia wananchi.
Nae, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Dk. George Lugomela amesema kwa sasa wizara hiyo imeanza mpango wa kujenga na kukarabati mabwawa hasa maeneo yenye ukame mkubwa na wilaya ya Maswa ikiwemo.
Amesema ujenzi wa mabwawa hayo mawili wilayani humo ni utekelezaji wa mipango madhubuti ya serikali kusimamia, kutunza, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za maji kwa matumizi bora na endelevu kwa kuhakikisha usalama wa maji.
“Kila wilaya kuwa na angalau bwawa moja kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa maji unafikia asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini, hivyo serikali itaendeleza juhudi hizo na ninyi wananchi mnapaswa kuvilinda hivyo vyanzo vya maji kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” amesema Dk. Lugomela.
Awali, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji bonde la Ziwa Victoria, Dk. Renatus Shinhu amesema kuwa ujenzi wa mabwawa hayo utatumia kiasi cha Sh bilioni 1.6 zilizotolewa na serikali na wao wakiwa wasimamizi wa ujenzi watahakikisha yanakamilika kabla ya msimu wa mvua za masika kuanza mwezi Desemba, mwaka huu.