Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Tano Mwera, amesema wazazi na walezi wa wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shule, wamekuwa kikwazo kikubwa kesi za watuhumiwa wanaowapa ujauzito huo kufikia hatua ya hukumu Mahakamani.
Amesema wazazi wamekuwa wakiwatorosha watoto wao pindi watuhumiwa hao wanapofikishwa mahakamani na wengi wao hudai watoto wao wametoroka jambo ambalo si kweli.
“Hadi kufikia Machi mwaka huu, wanafunzi 53 wa kike, shule za msingi 17 na sekondari 36 walikutwa na ujauzito wakiwa shuleni, kesi hizo zilipelekwa mahakamani lakini hadi leo hakuna kesi hata moja ambayo ambayo imetolewa hukumu kutokana na nyingi kuishia njiani kutokana na wazazi au walezi wa wanafunzi hao kumalizana na watuhumiwa nje ya mahakama,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa wilaya amesema aliamua kuanzisha kampeni ya Paza Sauti inayolenga kupiga vita mimba na ndoa za utotoni akishirikiana na Shirika la Amref Health Africa.
“Kampeni hii ilianza Machi mwaka huu, ambapo tunawafikia wanafunzi kwa kuwaelimisha wajitambue, wajithamini, pia tunawaelimisha wazazi umuhimu wa kutoa ushirikiano mahakamani,” amesema.