FLORENCE SANAWA, MTWARA
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kufanya kazi kwa ushirikishwaji na kuweka wazi shughuli zinazofanywa na taasisi hizo ili jamii iweze kuelewa na kushirikishwa kwenye uwajibikaji.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa maua unaoendeshwa na shirika la Door of Hope to Women and Youth Tanzania amesema kuwa mashirika yanapaswa kufanyakazi kwa kasi kwa ubora unaotakiwa na kuhakikisha kuwa jamii wanayoihudumia inafahamu shughuli wanazozifanywa.
“Zipo taasisi zisizo za kiserikali nyingi zinafanya kazi kwa kujipenyeza hali ambayo inasababisha wengi wao kukamatwa ni kwasababu huwa wanaingia kama wezi unakuta hakuna mtu anaejua wanafanya nini malengo yao nini hata ukiwauliza wanakuwa wakali,” amesema.
“Asasi zinapaswa kuelewa kuwa utaratibu wa kufika na kutoa maelekezo kwa uongozi wa eneo ulilopo inasaidia jamii kujua umuhimu ndio maana tunahitaji asasi zenye ushirikishwaji wa hali ya juu ili wananchi waweze kushiriki pia njia mojawapo ya kukaribishwa kwenye maeneo husika.” amesema Mmanda.