24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

DC ashtukia utoroshaji dhahabu

ELIUD NGONDO -CHUNYA

ZAIDI ya nusu ya madini ya dhahabu yanayonunuliwa na wanunuzi wa kati kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo wilayani Chunya, inatoroshwa badala ya kupelekwa soko kuu la dhahabu lililofunguliwa na Serikali.

Akizungumza na wanunuzi wa dhahabu wilayani Chunya jana, Mkuu wa wilaya hiyo, Maryprisca Mahundi, alisema wamefanya uchunguzi na kubaini kiasi kikubwa cha dhahabu kinanunuliwa kutoka kwa wachimbaji wadogo, lakini hakipelekwi sokoni.

Alisema licha ya soko la madini lililofunguliwa wilayani humo tangu Mei 2, mwaka huu kufanya vizuri, imebainika kiasi kikubwa cha dhahabu inayouzwa sokoni hapo inatoka viwanda vya uchenjuaji.

“Tumefanya uchunguzi, tumegundua dhahabu nyingi inayouzwa kwenye soko letu ni ile inayotoka kwenye ‘illusion’ ambayo ni kiasi kidogo.

“Tumebaini kiasi kikubwa cha dhahabu inayonunuliwa na ‘brokers’ (wanunuzi wa dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo), hailetwi sokoni, badala yake inatoroshwa,” alisema Maryprisca.

Alisema katika uchunguzi huo, tayari amepata orodha ya wanunuzi wote wanaotorosha madini nje ya wilaya na kuwataka kila mmoja kwa nafasi yake ajieleze kwanini anatorosha madini na kuikosesha Serikali mapato.

Maryprisca alisema kitendo hicho pia ni cha uhujumu uchumi na kuwaonya wanunuzi hao kuacha tabia hiyo mara moja.

“Ninayo orodha ya wafanyabiashara wanaotorosha madini yetu, wapo wanaopitia Tabora kwenda Dar es Salaam na wengine wanadiriki hata kupanda ndege kuyapeleka Dubai, acheni mara moja tabia hiyo,” alisema Maryprisca.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Chunya, Luitufyo Mwambungu, alisema utoroshaji huo una harufu ya kuambatana na vitendo vya rushwa.

Ofisa Madini Mkazi wa Wilaya ya Chunya, Gibson Kamihanda, aliwataka wale wote wanaojihusisha na utoroshaji wa dhahabu kuacha tabia hiyo mara moja.

Alisema kwa mujibu wa sheria, mtu akikutwa anatorosha madini, hatua ya kwanza madini yake yatataifishwa, kulipa faini ambayo ni mara tatu ya thamani ya madini aliyokutwa nayo na tozo zote ambazo zingelipwa.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wilaya ya Chunya, Osaund Mbilinyi, alidai ipo changamoto ya wanunuzi na wachimbaji wa madini kutokuwa na mwitikio wa kulipa kodi.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles