Na TIMOTHY ITEMBE – TARIME
MKUU wa Wilaya Tarime, Glorius Luoga ameufunga kwa muda usiojulikana Mgodi wa Dhahabu wa Kibaga katika Kijiji cha Kebaga Kata ya Kenyamanyori kwa madai ya kutozingatia masharti ya uchimbaji madini nchini.
Akifunga mgodi huo juzi, Luoga alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali kuwa wachimbaji wa mgodi huo wanaendesha shuguli hizo kinyume cha utaratibu bila kuzingatia masharti ya uchimbaji ikiwa ni pamoja na kuwanyanyasa wafanyakazi.
“Mgodi huu una shida ya kulipa ushuru kwa halmashauri bado hawajalipa, lakini wao wenyewe wanagombana kutokana na kukosa utaratibu mzuri wa kugawana mawe yanayotoka ndani ya mgodi.
“Sasa wakae watatue matatizo haya ili wenye mashimo wapate haki yao, wenye viwanja na hata wale wenye milipuko,” alisema.
Alisema amesimamisha uzalishaji wa mgodi huo na kuacha kazi ya kina mama ambao wamekuwa wakiokota mabaki ya mawe.
Alionya kuwa kuanzia sasa hawataruhusiwa kuingia ndani ya shimo hadi watakapokubaliana na kufuata taratibu nzuri na kurejea kwake kumueleza wamekubaliana ikiwa ni pamoja na kulipia ushuru wa halmashauri.
Kamishna Masaidizi wa Madini Mkoa Mara, Nyaisaro Mugaya, alisema alikuwa akitembelea wachimbaji hao kwa muda ikiwamo kukaa nao mara kadhaa kwa kuwataka kutatua mgogoro wao ambao ulikuwa ukihatarisha amani lakini hali hiyo ilishindikana.
Mugaya alisema alifika mara kwa mara na kujadiliana nao lakini bado walishindwa kuzingatia makubaliano ambayo walikubaliana.
Alisema kila alipoondoka waliendelea na mambo yao hivyo kuendelea kwa mgogoro.
Katika hatua nyingine, Septemba 20, mwaka huu Diwani Kata ya Kenyamanyori, Ganga Mugendi (CCM) Halmashauri ya Mji wa Tarime alivamiwa na kukatwa mapanga kichwani.
Alilazwa katika Hospitali ya Bomani baadaye kuhamishiwa Bugando, Mwanza.