25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

DAYOSISI KKKT YAMKINGIA KIFUA MALASUSA


Na MWANDISHI WETU – Dar es salaam    |

WAKATI waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wakisubiri hatua itakayochukuliwa dhidi ya Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Dk. Alex Malasusa, Halmashauri Kuu ya dayosisi hiyo imeonyesha kumkingia kifua.

Hali hiyo imeonekana kutokana na barua iliyoandaliwa na Halmashauri Kuu, inayotarajiwa kusomwa leo kwa washarika wa dayosisi hiyo.

Kwa mujibu wa nakala ya barua hiyo ambayo MTANZANIA Jumapili imeipata, Halmashauri Kuu ya Dayosisi hiyo, imesema haikuwa na lengo la kupingana na maazimio ya Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) juu ya kusomwa kwa Waraka wa Pasaka.

Barua hiyo imesema maelekezo yote yaliyotolewa yamezingatiwa na imesisitiza kuwa umoja na mshikamano kwa Askofu Dk. Malasusa utaendelea katika kuongoza na kuihubiri Injili ya Yesu Kristo.

Chanzo cha kuaminika cha gazeti hili, jana kililionyesha nakala ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa DMP, Godfrey Nkini, iliyoelekezwa kusomwa leo katika ibada za dayosisi hiyo.

Barua hiyo ilieleza kuwa halmashauri hiyo ilikaa kikao Mei 2, mwaka huu na ilijadili na kujiridhisha kuhusu barua aliyoandikiwa Askofu Malasusa kuwa alikiuka mapatano yaliyotolewa na mkutano wa maaskofu wa KKKT.

“Halmashauri Kuu imetafakari kwa kina jambo hili na kujiridhisha kwamba: Haikuwa lengo la DMP kupingana na maazimio ya Mkutano wa Maaskofu daima. Maelekezo yote yaliyotolewa na KKKT Makao Makuu yamezingatiwa.

“Hata hivyo, Halmashauri Kuu imesikitishwa kwa jinsi suala zima lilivyotunzwa hadi kufikia vyombo vya habari na baadhi yao kupotosha ukweli wa suala zima,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Kuhusu Askofu Malasusa barua hiyo ilisisitiza: “Washirika mfahamu kwamba Malasusa ni Askofu wa DMP. Halmashauri inatoa pole nyingi kwa Baba Askofu na familia yake kwa usumbufu uliojitokeza. DMP itaendelea na umoja na mshikamano na Askofu Malasusa katika kuongoza na kuhubiri Injili ya Yesu Kristo.”

Pamoja na barua hiyo kutoa pole kwa washirika wote kutokana na kuumizwa kwao na taarifa za kuandikiwa barua Askofu Malasusa za kukiuka mapatano ya Baraza la Maaskofu, ilizodai haikuwa lengo la KKKT Makao Makuu kuwaumiza waumini wake, pia ilieleza inaendelea kulifuatilia jambo hilo kwa makini.

Pia barua hiyo iliwaelekeza washirika hao kuwa watulivu na kuliombea kanisa pamoja na kutunza amani na umoja.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Nkini kuthibitisha kuhusu barua hiyo, lakini hakuweza kupokea simu na alipotumiwa ujumbe mfupi kuwa kuna jambo linahitaji ufafanuzi, alimwelekeza mwandishi kununua gazeti la Upendo linalotoka leo.

“Niko msibani. Soma gazeti la Upendo. Upendo ni gazeti letu la Dayosisi limetoka leo (jana). Pita katika Usharika wowote wa KKKT utalipata, pia hata kwa wauza magazeti yanapatikana,” aliandika Nkini.

Pia MTANZANIA Jumapili lilimweleza nia ya kumtafuta, lakini pia hakutoa majibu zaidi.

Hata hivyo, gazeti hilo halikupatikana kwa wauza magazeti, huku chanzo kingine kikisema kuwa huwa linatoka leo na si jana.

Pamoja na hayo, chanzo cha awali cha MTANZANIA Jumapili kilisema barua hiyo ni halisi na ndiyo itakayosomwa leo katika ibada.

Itakumbukwa hivi karibuni Baraza la Maaskofu wa KKKT lilimtenga Askofu Malasusa kwa tuhuma za usaliti.

Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili lilizipata na kuandika wiki iliyopita, zilisema uamuzi wa kumtenga Askofu Malasusa ulifikiwa na kikao cha Baraza la Maaskofu wapatao 25, lililoketi mjini Arusha, chini ya kiongozi wake ambaye ndiye mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk. Fredrick Shoo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo gazeti hili lilikuwa la kwanza kuziandika kwa kina, uamuzi huo wa kumtenga Profesa Malasusa ulitangazwa pia katika kikao cha Halmashauri Kuu ya KKKT cha siku mbili ambacho nacho kilikuwa kikifanyika Arusha na kuhudhuriwa na wajumbe wake ambao ni maaskofu, makatibu wakuu wa dayosisi zote na wakuu wa vitengo.

Kiini cha tuhuma hizo za usaliti dhidi ya Askofu Malasusa, kinaelezwa kuwa ni uamuzi wake wa kuzuia waraka wa Pasaka ulioandaliwa na maaskofu 27 wa Kanisa hilo, usisomwe DMP anayoiongoza.

Waraka huo ambao unadaiwa kumponza Profesa Malasusa, ni ule uliotolewa na kusainiwa na maaskofu, akiwamo yeye mwenyewe mwishoni mwa Machi, mwaka huu – wiki moja kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka.

Pamoja na mambo mengine, waraka huo uliogusa na kuonya mwenendo wa masuala ya uchumi, siasa na kijamii, uliamsha mjadala mkali ndani ya jamii na viongozi wa Serikali na kisiasa.

Ujumbe ambao Askofu Malasusa anatuhumiwa kumwagiza mmoja wa wasaidizi wake autume kwa wachungaji wa DMP anayoiongoza ukiwazuia wasiusome waraka huo Jumapili ya Pasaka unasomeka hivi:-

“Bw Yesu asifiwe. Viongozi. Tafadhali mnaombwa kuwajuza watumishi wote katika majimbo yenu kuwa inaelekezwa kwamba waraka wa Pasaka kutoka KKKT usisomwe wala kutajwa katika ibada au popote hadi hapo uongozi wa Dayosisi utakapotoa maelekezo.”

Taarifa zinaeleza katika kikao hicho, Askofu Malasusa, alipewa nafasi ya kujitetea na katika maelezo yake akasema aliona tayari waraka huo umesambaa vya kutosha katika mitandao ya kijamii na hivyo kuamini umekwishawafikia waumini wote.

Inaelezwa alipoulizwa kuhusu ujumbe anaotuhumiwa kuagiza utumwe kwa wachungaji ukiwakataza kuusoma waraka huo, Profesa Malasusa, alijibu si wake na kutaka aulizwe aliyeutuma.

Pamoja na Askofu Malasusa kutoa maelezo hayo, inaelezwa baadhi ya wachungaji wa DMP ndio waliopeleka kwenye Baraza la Maaskofu vielelezo vya barua, wakiwa wamezisaini na kuthibitisha walipewa maelekezo ya kutousoma waraka huo.

Gazeti hili liliwahi kuandika wiki iliyopita kuwa chini ya utaratibu wa kanisa hilo, inaelezwa pamoja na kwamba linaongozwa na Baraza la Maaskofu, lakini uamuzi wa kumvua uaskofu Malasusa uko chini ya Dayosisi anayoingoza ya DMP.

“Ataendelea kuwa askofu, lakini hatahudhuria kikao chochote wala uamuzi wowote wa Baraza la Maaskofu hatahusika nayo, na amepewa muda wa kutafakari kuhusu uamuzi huo hadi Septemba, mwaka huu na kisha arudi kuliomba radhi kanisa, sasa ni jukumu la Dayosisi ya Mashariki na Pwani kuona kama ni sahihi kuendelea au la na askofu aliyetengwa na Baraza la Maaskofu,” kilisema chanzo chetu kingine ndani ya kanisa hilo.

Pamoja na Malasusa, askofu mwingine wa kanisa hilo, Dayosisi ya Kusini Mashariki, Dk. Lucas Mbedule, yeye alitii maagizo ya Baraza la Maaskofu kwa kuwaomba radhi waumini.

Askofu huyo ni miongoni mwa maaskofu waliotuhumiwa kusaliti waraka wa Pasaka kwa kuzuia usisomwe katika dayosisi zao.

Katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya KKKT na kile cha Baraza la Maaskofu, Askofu Mbedule na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Solomon Massangwa, walitakiwa kuomba radhi.

Tukio la kuomba radhi kwa askofu huyo liliripotiwa kufanyika wakati wa ibada ya Jumapili iliyopita katika Kanisa la KKKT Usharika wa Mtwara Mjini.

Alisema alimwandikia barua Askofu Dk. Shoo na maaskofu wote wa kanisa hilo, huku akisema yuko pamoja na maaskofu wenzake kwa sababu alishiriki kuuandaa waraka huo.

Askofu huyo alisema alishindwa kuusoma waraka huo kwa sababu zilizojitokeza wakati huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles