SPIKA mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, amesema jitihada za kupambana na dawa za kulevya zinatakiwa ziongezwe kwa kuwa zinawaathiri wanafunzi wa shule za sekondari nchini.
Makinda aliyasema hayo jana wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, alipokuwa akizungumza wakati wa mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu St.Joachim.
“Matumizi ya dawa za kulevya katika shule za sekondari yamekuwa ya kawaida ingawa madhara yake ni makubwa katika jamii.
“Madawa hayo yanachangia maadili kumomonyoka kwani kuna baadhi ya vijana wa kiume wanalawitiana wenyewe kwa wenyewe.
“Hali kwa sasa si nzuri, yaani matumizi ya dawa hizo yameongezeka, ndiyo maana ninasema kuna haja ya kuongeza nguvu za kupambana na matumizi ya dawa hizo,” alisema Makinda.
Katika maelezo yake, Makinda alionyesha kusikitishwa na tabia ya watu wazima kuwabaka watoto wadogo, jambo ambalo alisema linatokea kwa sababu watu hawana hofu ya Mungu.
“Kwa sasa mtu mzima kumwingilia mtoto wake wa kumzaa kinyume na maumbile ni jambo la kawaida. Sasa ifike wakati jamii na viongozi wa dini tupaze sauti kwa sababu watoto wetu wako hatarini,” alisema.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Padri Deogratias Mchagi, alisema vijana wanatakiwa kuongeza bidii katika masomo kwa kuwa taifa linahitaji watu wenye elimu bora na maadili mema.
“Kwa sasa suala la elimu bora nchini bado lina changamoto ambapo nguvu kubwa zinahitajika ili tufike tunakotakiwa kufika,” alisema Padri Mchagi.