31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Guardiola na tatizo la kushindwa kuwasiliana na wachezaji

guardiolaADAM MKWEPU NA MITANDAO

MBALI ya kuwa kocha bora duniani, Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, anadaiwa kuwa na chuki binafsi dhidi ya wachezaji nyota anaowakuta katika timu anayohamia.

Kitendo hicho ndio sababu ya kocha huyo kukorofishana na wachezaji hao nyota mara kwa mara katika timu anayoifundisha.

Guardiola aliwahi kukorofishana na Zlatan Ibrahimovic, Cesc Fabregas na Samuel Eto’o, Ronaldinho Gaucho, Yaya Toure wakati akiwa kocha wa Barcelona, Franck Ribery akiwa Bayern Munich na sasa Yaya Toure kwa mara ya pili akiwa Man City.

Mchezaji wa Juventus, Medhi Benatia, ambaye aliwahi kucheza timu ya Bayern Munich kwa misimu miwili kipindi ikiwa chini ya Guardiola, anasema tabia ya kocha huyo ilitokana na vitendo vya baadhi ya wachezaji akiwa kocha wa Barcelona.

Benatia, ambaye kwa sasa anacheza  chini ya kocha wa Juventus, Max Allegri, alilieleza  jarida la Gazzetta la nchini Italia kuwa  kocha Guardiola na Allegri wanataka mchezaji kucheza mpira.

“Ni makocha ambao wapo tofauti Allegri yupo karibu sana na wachezaji, lakini Guardiola hana mawasiliano na wachezaji.

“Alinieleza kuwa sababu ya kuwa hivyo inatokana na kuchukizwa na tabia za baadhi ya wachezaji akiwa Barcelona, hivyo akaamua kufanya kazi yake kama kocha,” alisema Benatia.

Beki huyo anasema uhusiano mbaya wa kocha huyo na wachezaji wake umemfanya kujikita zaidi katika majukumu yake ya ukocha.

“Guardiola aliacha kuifundisha Barcelona kutokana na uhusiano mbaya dhidi ya wachezaji,” anasema Benatia.

Mmorocco huyo, ambaye alijiunga na Bayern Munich mwaka 2014 akitokea timu ya Roma akiwa chini ya Guardiola, alifanikiwa kushinda mataji mawili, likiwamo la Ligi Kuu na kombe la DFB-Pokal, kabla ya Agosti mwaka huu kuhamia Juventus kwa mkopo.

Naye beki wa zamani Munich ambaye kwa sasa anacheza timu ya Nice, Dante Bonfim, anathibitisha kwamba kocha huyo hana huruma kwa wachezaji wake.

Dante aliwahi kushinda mataji matatu mfululizo mwaka 2013 akiwa na kocha Juup Heynckes na kutumia mwaka mmoja kuwa chini ya kocha Guardiola kabla ya kuhamia timu ya Wolfsburg na baadaye Nice.

Mbrazili huyo anaamini kwamba Guardiola hana uwezo wa kuwaunganisha wachezaji kuwa kitu kimoja katika timu.

“Hana muda wa kuzungumza na wachezaji, hivyo kama mchezaji unakuwa hajui upo katika hali gani ukiwa chini yake.

“Wapo makocha ambao kimbinu wanaonekana kuwa bora lakini hawana tabia za kibinadamu kama ilivyo kwa Guardiola,” anasema Dante.

Winga wa Bayern Munich, Arjen Robben, anafunguka kwa kusema kuwa kuna tofauti kubwa kati ya Guardiola na kocha wa sasa wa timu hiyo, Carlo Ancelotti.

“Unatakiwa kuwa makini unapowaelezea makocha hawa wawili, kwani kila mmoja ana tabia zake, lakini nina furaha zaidi nikiwa chini ya Ancelotti,” anasema Roben.

Kwa upande wa kipa wa zamani wa Manchester City ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo katika timu ya Torino, Joe Hart, anasema hana uwezo wa kubadili mawazo ya kocha huyo kwa kile anachoamini katika soka.

“Soka ni mchezo wa  maoni na  watu wengine wana maoni kuhusu mimi na wengine wanahisi sifai kuwa kipa wa Manchester City.

“Kuna wakati maoni ya watu yanaweza kuwa mabaya au mazuri, lakini ninachoangalia ni kazi yangu,” anasema Hart.

Hart anasema kinachomfanya kocha huyo kuendelea na vitendo vya chuki kwa wachezaji inatokana na anavyoamini katika mafanikio yake tangu akiwa Barcelona na Munich.

Hata hivyo, kwa sasa Guardiola yupo katika presha baada ya kucheza micheza minne bila ushindi, huku  mfumo wake ukikosolewa na mashabiki wa timu hiyo.

Walitoka sare dhidi ya Celtic katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kabla ya kupoteza dhidi ya Tottenham Hotspur ambao ulikuwa mchezo wa kwanza kuchapwa wa Ligi Kuu England.

Kocha huyo pia alipata matokeo ya sare dhidi ya Everton ambayo ilifuatiwa na kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Barcelona katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, Guardiola anasema yupo tayari kurudi kwao Hispania  kuliko kubadili mfumo wake ndani ya timu hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles