Wamshangaa na kumkumbusha kauli yake ya kumtambua Maalim Seif
Na EVANS MAGEGE
SIKU moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kusema hafanyi kazi na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, upande wa chama hicho unaomuunga mkono katibu mkuu huyo, umeibuka na kumhoji Spika maswali matano huku wakimkumbusha kauli yake aliyowahi kuitoa ya kumtambua Seif.
Maelezo hayo yalitolewa na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Salim Bimani, jana alipokuwa akizungumza na MTANZANIA Jumamosi.
“Wakati wa kugombea ubunge wa Afrika Mashariki alitamka bungeni kuwa CUF ina matatizo.
“Akasema kuna CUF ‘A’ na CUF ‘B’ na akampokea Twaha Taslima ambaye alikuwa mgombea halali aliyepitishwa na kikao halali cha Baraza Kuu chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif.
“Pia akapokea wagombea hao haramu waliopelekwa na huyo Msajili ambao walipitishwa kutokana na Barua ya Profesa Lipumba (Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na msajili Profesa Ibrahim Lipumba). Hawa wote akawaruhusu waingie katika uchaguzi,” alisema.
Alisema kama Spika wa Bunge hawezi kufanya kazi na Katibu Mkuu wa CUF, ndani ya Bunge wapo wabunge wanaomuunga mkono Maalim Seif, hivyo awatoe wote.
“Ndugai alifanya maamuzi bila kufanya tafiti, chama kina kesi mahakamani dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Huwezi kufanya maamuzi mengine yoyote bila kwanza kutumia hekima tu na busara kusubiri kuuliza angalau huku ni kwema?
“Hili suala liko kwenye mahakama na Katibu Mkuu amechaguliwa na Mkutano Mkuu mwaka 2014. Hivyo chombo kinachoweza kumwondosha ni Mkutano Mkuu wa Taifa.
“Makao Makuu ya Chama yako Zanzibar, Dar es Salaam ni Ofisi Kuu. Katibu Mkuu ni Taasisi, huwezi kusema Katibu Mkuu hajaenda Buguruni alafu ukapanga nafasi yake akaimishwe mtu… Huo ni uvurugaji na uuaji wa demokrasia katika vyama vya siasa,” alisema Bimani.
Bimani pia alihoji ikiwa Bunge linatunga sheria ikiwamo ya Vyama vya Siasa, je, Spika alijiridhisha kwenye Katiba ya CUF kama kuna Kaimu Katibu Mkuu?
Bimani aliendelea kuhoji kwamba hata kama Spika amejitetea kuwa anapewa taarifa na Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini hakuona kama msajili ameshtakiwa mahakamani?
“Kwanini alifuata matakwa ya Msajili? Yani Msajili anamwingiza kwenye shimo na yeye anaingia?” alihoji.
Alichosema Ndugai juzi
Akizungumza na waandishi juzi katika ofisi ndogo za Bunge zilizopo Dar es Salaam, Ndugai alisema hawezi kufanya kazi na Maalim Seif kwa sababu hayupo ofisini hivyo nafasi yake inakaimiwa na mwingine.
Alisema msimamo huo ni suala la utaratibu kwa sababu mwenye kumbukumbu za vyama vya siasa na viongozi wake halali ni Msajili wa Vyama vya Siasa, hivyo kama msajili akisema hamfahamu mtu na yeye lazima asimfahamu.
“Kwa hiyo linapotokea jambo kwenye chama ambacho kina mvutano, kazi yangu ni kumuuliza huyo mweka hazina wa vyama vya siasa kwa maana hiyo niliyoieleza kwamba ‘kuna huyu’, ‘aah huyu simfahamu’ basi na mimi nakuwa simfahamu. Akisema namfahamu basi na mimi nakuwa namfahamu.
“Lazima twende kwa utaratibu, ni sawa na taasisi fulani ambayo inatakiwa iandikishwe Brela (Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara) mnanielewa? Ikatuandikia Bunge jambo fulani, lazima tuiulize Brela ‘bwana unamjua huyu’? Akisema hatumjui maana yake na mimi simjui.
“Sasa siwezi kuzuka nikawa nawatambua watu ambao hawatambuliwi na Brela, kwa maana hiyo ya makampuni na kadhalika, siwezi kuwatambua watu ambao hawatambuliwi na msajili kwa sababu huko ndiko vyama vinakopeleke Katiba zao, huko ndiko vyama vinakopeleka mabadiliko ya kumbukumbu zao za mikutano ya mabadiliko yoyote yale,” alisema Ndugai.
Alisema Machi mwaka huu alipata barua kutoka kwa Msajili iliyomweleza kwamba amepata taarifa rasmi kuwa Maalim Seif Hamadi hayupo ofisini, hivyo majukumu ya chama hicho yatatekelezwa na Naibu Katibu Mkuu wake hadi hapo itakapoelezwa vinginevyo.
“Huo ndio msimamo wa tangu Machi kwa mujibu wa barua niliyokuwa nimeandikiwa kama rekodi ya kufanyiwa kazi, sasa ninapoletewa barua na mtu huyo baadaye ungekuwa wewe ungefanyaje?
“Wakati umekwishaharifiwa kwamba huyo mtu hayupo ofisini, sasa swali la kwanza ni kumuuliza huyo mtu amesharudi ofisini? Akikwambia hapana sasa barua naandikia wapi, Kongwa? (Kwenye Jimbo la Ndugai).
“Kwa hiyo inakuwa ngumu kidogo. Ni tatizo la kwao hamuwezi kumlaumu Spika au mtu mwingine. Ni usafi wa kufanya ndani kwao wenyewe, wakifanya usafi wao sisi wala hatuna tatizo.
“CUF ikisema inakutambua wewe sisi tutapinga? Hili ni la kwao na wanajua zaidi wao kuliko sisi, tuwaachie wao wenyewe jukumu la kusafisha nyumba yao,” alisema Ndugai.