24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

LIGI KUU BARA 2017/18 KILA MTU ATAPAMBANA NA HALI YAKE

NA WINFRIDA MTOI

KIPENGA cha Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/2018 kimepulizwa ambapo leo michezo mbalimbali itapigwa katika viwanja tofauti huku mechi moja ikitarajiwa kuchezwa kesho.

Katika kuashiria kama pazia hilo la Ligi Kuu limefunguliwa, ni baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ngao ya Jamii uliowakutanisha mahasimu wa muda mrefu Simba na Yanga.

Msimu huu ni kama ule uliopita ambao utashirikisha timu 16, tatu zikiwa ni mpya zilizopanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza ambazo ni Singida United yas mkoani Singida, Lipuli FC ya Iringa na Njombe Mji.

Katika kipindi cha usajili tuliona mchuano ulivyokuwa mkali kila timu ikihaha kuimarisha kikosi chake na baada ya hapo tukashuhudia maandalizi tofauti yakitegemea uwezo wa kifedha wa klabu.

Hapa unaona ni jinsi gani msemo wa pambana na hali yako ulivyodhihirika kwani yule aliyekuwa na kisu kikali yaani fedha ndiye aliyeweza kupata wachezaji waliokuwa wanazitoa udenda timu nyingi.

Timu nne za Simba, Yanga Azam FC na Singida United zimeonekana kupambana vikali katika eneo hili la usajili ambapo walifanya kuviziana kuchomoa wachezaji kwenye baadhi ya timu.

Kati ya hizo Simba inashika namba moja kwa kufanya usajili mkubwa na kuchukua wachezaji wengi nyota kutokana na kipato chao cha fedha kuwazidi wengine.

Usajili huo utairudisha Simba iliyopotea kwa misimu kadhaa na kukosa ubingwa kwa miaka mitano mfululizo na kuondoka katika ramani ya soka la kimataifa kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya kushiriki kwa muda wote huo.

Nyota wapya wanaoangaliwa kwa jicho la tofauti na mashabiki wa soka kwa kuamini watarudisha hadhi ya Simba ni Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Aishi Manula na John Bocco.

 

Wengine ni Shomary Kapombe,  Erasto Nyoni, Salim Mbonde, Ally Shomary, Said Mohamed ‘Nduda’, Jamali Mwambeleko, Emmanuel Mseja, Yusuph Mlipili na Mghana Nicolaus Gyan.

Ukiachana na Wekundu hao wa Msimbazi, timu nyingine iliyopania kufanya maapinduzi katika ligi msimu huu ni Singida United, timu iliyopanda daraja lakini imeingia kwa kishindo na kufanya usajili mkubwa.

Singida United imeingia kwenye orodha ya timu zitakazoleta ushindani katika Ligi Kuu huku mashabiki wengi wa soka wakiitazama kama timu iliyokuja kuzipa changamoto klabu kongwe.

Timu hii katika kuonyesha kwamba imepania kufanya kweli, imeweza kusajili idadi ya wachezaji saba wa kigeni kama inavyotakiwa ikiwamo mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita Rwanda, Danny Usengimana.

Nyota wengine wa kigeni watakaoonekana katika kikosi hicho ni  Elisha Muroiwa, Nhivi Simbarashe (Zimbabwe), Wisdom Mtasa, Tafadwaza Kutinyu, Shafik Batambuze (Uganda), Michael Rusheshangoga.

Singida ikiwa chini ya kocha Mholanzi, Hans van de Pluijm, aliyekuwa Yanga zamani, pia imesajili wachezaji wazawa ambao ni Kenny Ally, Ali Mustapha ‘Bathez’, Pastory Athanas, Atupele Green na Miraji Adam.

 

Kwa upande wa mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga iliyotwaa ubingwa mara 26, itaanza kucheza na Lipuli FC, msimu huu inaingia ikiwa haijafanya usajili wa kufuru kama ilivyozoeleka na hiyo ni kutokana na ukata uliokuwa unawakabili.

Hata hivyo, kwa wachezaji hao wachache waliowasajili, inaonekana wamezingatia zaidi mahitaji ya kikosi chao kwa kuziba zile nafasi zilizoachwa wazi na sehemu zilizoonekana kuwa dhaifu msimu uliopita.

Kwa misimu mitatu Yanga ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kiungo wa nyuma, lakini ujio wa Kambamba Tshishimbi kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland na kiwango alichokionyesha katika mechi ya Ngao ya Jamii, kinawapa Wanayanga matumaini ya kufanya vizuri kwenye ligi msimu huu.

Kwa ujumla kikosi cha Yanga kwa msimu huu kinakuwa na wachezaji sita wapya ambao ni makipa wawili, Youthe Rostand, Ramadhan Kabwili, walioziba mapengo ya Deogratius Munishi na Ally Mustapha ‘Barthez’.

Wengine ni Abdallah Shaibu Haji “Ninja, Raphael Daud, Baruani Akilimali, Ibrahim Ajib na beki Gadiel Michael.

Kikosi cha Azam FC kinachonolewa na Mromania, Aristica Cioaba, nao msimu huu wamekuja kivingine kutengeneza muundo mpya wa kikosi chao ambacho kitatawaliwa zaidi na vijana.

 

Ukiangalia safu nzima ya ushambuliaji imeshikwa na vijana, Mbaraka Yusuf, Wazir Junior, Yahya Zayd na Shaban Idd wakiongozwa na mkongwe raia wa Ghana, Yahya Mohammed.

Uamuzi wa Azam kuwaruhusu wachezaji wake wengi kuondoka akiwamo kipa namba moja, Aishi Manula, kulizua maswali mengi kwa wadau wa soka na kuamini kuwa kikosi hicho kinapotea.

Lakini baada ya kuchukua nyota hao wadogo na kuwachanganya na wakongwe, picha halisi kuelekea Ligi Kuu imeanza kuonekana hasa baada ya maandalizi waliyofanya huku wakicheza mechi za kirafiki nje na ndani ya nchi.

Hata hivyo, wapo ving’ang’anizi wa Ligi Kuu ambao hawatabiriki, muda wowote wanabadili mwelekeo wa matokeo yao kwa kupigania nafasi walizokusudia, timu hizi ni Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons na Kagera Sugar.

Mfano mzuri ni msimu uliopita, Kagera Sugar iliweza kujihakikishia nafasi ya tatu na kufanikiwa kufanya hivyo huku ikitoa mchezaji bora chipukizi Mbaraka na kocha bora, Meck Mexime ambaye ndiye anakinoa kikosi hicho hadi sasa.

Timu hizi huwa hazina mbwembwe nyingi za usajili kwani hata wale walioachwa kwao ni sawa ila ligi inapoanza huwa hawakubali kuburuzwa kirahisi, Mtibwa Sugar itakua chini ya kocha Zubery Katwila, Tanzania Prisons na Abdallah Mohamed.

Kuna wale waliozoea kushika mkia nao bado wamo ni Ndanda FC na Majimaji ambao msimu uliopita pamoja na Mbao FC ziliponea chupuchupu kushuka daraja kwa kuokolewa na ushindi wa mechi za mwisho.

Pia zipo timu za Mbeya City, Ruvu Shooting na Stand United,  matokeo yao yamekuwa yakipanda na kushuka na mara nyingi wamekuwa wakikamia mechi kubwa.

Kulingana na usajili na maandalizi ya timu zote mtanange wa ligi unatarajiwa kuwa wa tofauti na misimu mingine kutokana na ushindani unaopanda siku hadi siku kila mmoja akiingia kwa kutaka nafasi za juu.

Wadhamini walijitokeza kwenye baadhi ya timu pia imekuwa ni chachu ya kila mmoja kutaka kuonyesha uwezo ili kuendelea kutunisha mfuko kupitia wadau hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles