28.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

WEKA MISINGI IMARA YA MAISHA YA WATOTO WAKO

Na ATHUMANI MOHAMED

NI siku nyingine tena tunakutana katika safu yetu hii ambayo tunapeana madini kuhusu maisha. Ndugu zangu katika maisha ukikubali kusikiliza hata yale usiyoyapenda inakuwa rahisi zaidi kufanikiwa kuliko kusikia yale ambayo unayapenda pekee.

Unaweza kuwa na marafiki wengi, lakini wanakukubalia kila kitu. Kila unapokutana nao wanakumwagia sifa kutokana na mambo mbalimbali.

Wote wanakueleza mazuri tu, hakuna anayekukosoa hata mmoja. Ukiona una marafiki wengi wa namna hiyo, ujue  siyo sahihi. Rafiki sahihi ni yule anayekuambia ukweli hata pale unapokosea.

Ukweli Kuhusu Maisha ni safu ambayo hueleza watu ukweli ili uwasaidie kubadilisha maisha yao. Bila shaka kwa kuelezwa ukweli itakusaidia kujua namna gani ya kutoka ulipo na kusonga mbele.

Ndugu zangu tunapaswa kuandaa maisha ya baadaye ya watoto wetu. Siyo jambo zuri kuwaacha watoto walelewe na dunia, wakati ni wajibu wa wazazi kuhakikisha mtoto anakuwa nani baadaye kulingana na mazingira unayoandaa kwa mwanao huyo.

Wapo baadhi ya wazazi huwalea watoto wao katika mazingira ambayo ni kama kesho wataendelea kuwa nao. Mjenge mwanao aweze kuishi kwa kujitegemea mwenyewe hata kama ukiwa haupo.

Jiulize, utaishi milele na watoto wako? Kumbuka kuna utu uzima. Mtoto akifikisha kuanzia miaka 20 atakuwa ameshaanza kukaa peke yake.

Wapo baadhi ya watoto huanza kuishi maisha ya boarding kuanzia kidato cha kwanza. Maana yake, umri wa mtoto huyo utakuwa umeshagonga kuanzia miaka 14 – 16.

Hadi kufikia miaka 22 – 26 atakuwa anamaliza elimu yake ya juu akiwa anaishi na watu wengine. Wachache baada ya kumaliza elimu ya juu hurudi majumbani mwao.

Wengi huanzisha maisha yao (hasa wavulana) na pengine hupata kazi au kuamua kujiajiri mbali na nyumbani (nje ya mkoa wanaoishi wazazi wake).

Kinachotokea hapo ni kuanza kupambana na maisha yake akitumia mbinu ambazo ulimwandalia wakati unaishi naye. Je, ulisimama sawasawa?

 

KAZI ZA NYUMBANI

Tatizo usasa, umaridadi na maisha mapya. Wazazi wengi wa sasa (na hasa wa mijini) huishi na wadada wa kazi ambao husaidia kazi za nyumbani. Watumishi hawa wa ndani wameachiwa majukumu yote.

Kwa sababu dada huyo analipwa (siyo pesa nyingi, wengi hulipwa Tsh. 50,000) basi anaachiwa kila kitu. Unakuja kushangaa mtoto mkubwa anayesoma darasa la sita hajui kufua hata boksa yake! Ni mambo ya aibu na upuuzi kabisa.

Mfundishe mtoto wako kufua nguo zake mwenyewe. Ni kweli mtoto anaweza asiwe mzuri sana kwenye kufanya kila kitu, lakini angalau ajue kufua nguo zake za kushindia.

Akishazoea kufua za kushindia, baadaye ataongeza juhudi na kujikuta akifua mwenyewe. Mfundishe kunyoosha nguo zake mwenyewe na kusafisha viatu vyake.

Jambo hilo ni la muhimu sana. Inatakiwa mtoto anapofika darasa la saba awe ameshajua kufua vizuri nguo zake zote. Kadhalika awe ameshajua (japo kwa kiasi) kupika baadhi ya vyakula.

Hiyo itamsaidia hata atakapokwenda kusoma shule za bweni, maisha yake hayawezi kuwa magumu. Hatakuwa mtoto wa kudeka hovyo, maana kila kitu anakijua.

 

ELIMU YAKE VIPI?

Je, unamfuatilia mtoto wako maendeleo yake ya shule? Kama ulikuwa unajisahau anza sasa kumfuatilia mtoto wako. Fahamu maendeleo yake ya shule kwa kukagua daftari zake angalau mara moja kwa wiki.

Kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na walimu wake, itakusaidia kujua maendeleo ya mwanao. Acha kudharau maendeleo ya mwanao. Hata kama una fedha kiasi gani, hazitakuwa na maana kama mwanao hatakuwa na elimu nzuri.

Anaweza kuwa anafaulu vizuri masomo yake, lakini akawa na tabia nyingine mbaya. Kwa kuwa karibu na walimu na hasa mwalimu wa darasa, itakusaidia kufahamu maendeleo ya mtoto wako.

Maisha ya kesho ya mtoto yanajengwa na mzazi. Usiiachie dunia ikulelee mwanao.

Kwa leo naishia hapa, wiki tutaendelea. Wako katika mafanikio, Athumani Mohamed. Wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles