26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yaingiza wamiliki wa magari ya abiria matatani

ALLAN VICENT

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA) mkoani Tabora, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali wamekamata magari 20 ya abiria kwa kukaidi kupulizia dawa ya kuzuia virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu.

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka hiyo mkoani hapa, Neslon Mmari, alisema magari hayo yamekamatwa baada ya wamiliki kukaidi agizo la Serikali linalowataka kuhakikisha magari yao yanapuliziwa dawa hiyo kabla ya kuanza safari ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.

Alisema katika operesheni hiyo pia walibaini kuwa baadhi ya vyombo vya usafiri vimeendelea kujaza abiria kupita kiasi jambo ambalo ni kinyume na maelezo ya Serikali ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema gari lolote litakalokaidi maelekezo yoyote ya Serikali katika kipindi hiki ikiwemo kutopulizia dawa ya kuzuia maambukizi ya virusi hivyo halitaruhusiwa kuendelea na safari na litakamatwa.

Kwa upande wao baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri na madereva walisema hawajakaidi maelekezo ya Serikali ila tatizo ni upatikanaji wa vifaa hivyo.

Walisema wako tayari kupulizia dawa katika magari yao ila wakaomba wapuliziaji wawe wanapatikana kiurahisi ili kuepusha usumbufu usio na sababu na risiti zao za malipo ziwe ni zile zinazotambulika na mfumo wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ili kuepusha malalamiko.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, akizungumza katika wa kongamano la elimu ya kujikinga na virusi vya corona aliitaka wakiwemo wamiliki wa vyombo vya usafiri kufuata maelekezo yote yanayotolewa na viongozi na maofisa wa taasisi za serikali.

Alionya kuwa yeyote atakayekaidi kufuata maelekezo yoyote yanayotolewa hasa katika kipindi hiki  au kujaribu kukwamisha jitihada hizo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha aliwakumbusha wamiliki wa vilabu vya pombe za kienyeji na baa kutoruhusu msongamano wa aina yoyote ile katika maeneo yao na kuonya kuwa atakayeenda kinyume na maelekezo hayo atakamatwa na baa yake itafungwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles